Jamaa kutoka Kakamega amuua kakake katika ugomvi kuhusu mlo wa ugali-omena

Adamba alipigwa na kifa butu kichwani akaanguka na kupoteza fahamu.

Muhtasari

•Wawili hao walizozana baada ya Kilibwa kutaka kupewa omena zaidi, jambo ambalo Adamba aliipinga.

•Kaka yao mkubwa, Vincent Misango, 56, aliingilia kati lakini Adamba akampiga na kitu butu kichwani akaanguka na kupoteza fahamu. 

Mlo wa Ugali-Omena
Image: MAKTABA

Polisi katika kaunti ya Kakamega wanamzuilia jamaa mmoja kwa madai  ya kumuua kaka yake kufuatia mzozo wa chakula.

Ndugu wawili waliotambulishwa kama  Albert Adamba na John Kilibwa walizozana kuhusu mlo wa ugali na omena ambao walikuwa wamepewa na mama yao  kama chajio mnamo Jumapili usiku.

Tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Kambi Elijah, eneo la Likuyani, kaunti ya Kakamega.

Wawili hao walizozana baada ya Kilibwa kutaka kupewa omena zaidi, jambo ambalo Adamba aliipinga.

Kaka yao mkubwa, Vincent Misango, 56, aliingilia kati lakini Adamba akampiga na kitu butu kichwani akaanguka na kupoteza fahamu. 

Misango alikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Turbo ambako alitangazwa kuwa amefariki alipowasili. Majirani walisema ndugu hao watatu wamekuwa wakizozana kuhusu kipande cha ardhi kwa muda mrefu.

 "Wamekuwa hawakubaliani kuhusu jinsi wanavyopaswa kugawana kipande cha ardhi kilichoachwa na marehemu baba yao," mzee wa kijiji Jimmy Kwayumba alisema. 

Chifu msaidizi wa Seregeya Moses Wanjala alithibitisha kuwa mshukiwa alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Likuyani na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanzishwa. 

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Mochari ya Kimbilio kaunti ya Uasin Gishu. Wakati huohuo, mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 41 uligunduliwa ukioza nyumbani kwake baada ya kudaiwa kuuawa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Kilimani, kitongoji cha Seregeya, kaunti ndogo ya Likuyani. 

 Mjomba wa marehemu Reuben Mielizu alisema washambuliaji waliiba pesa taslimu kabla ya kutoroka kupitia dirishani.

“Walimnyonga kwa kutumia kitambaa cha mezani, ambacho tulikuta bado kimefungwa shingoni mwake. Baada ya mauaji hayo, walifunga mlango kutoka ndani na kutoroka kupitia dirishani,” Mielizu alisema. 

Chifu msaidizi wa eneo hilo Moses Shivina alisema marehemu alihamia eneo hilo hivi majuzi baada ya kuuza ardhi yake katika kijiji cha Munyama, lokesheni ya Lumakanda, kaunti ndogo ya Lugari. 

Shivina alisema marehemu alikuwa bado na pesa taslimu kutokana na mauzo ya ardhi hiyo, ambayo inaaminika kuwa lengo la wauaji wake. Alisema majirani walipatwa na wasiwasi baada ya kushindwa kumuona kwa siku tatu. 

Mmoja wao alikwenda kuangalia nyumba yake na kukuta mlango umefungwa kwa ndani. Alisukuma dirisha moja na kugundua mwili ukiwa juu ya kitanda. 

Mwili wa marehemu ulitolewa na kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya Kimbilio kaunti ya Uasin Gishu. 

Maafisa kutoka idara ya DCI wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.