Kamishna Msaidizi wa kaunti alipatikana amefariki katika nyumba yake Kirinyaga

Marehemu alikuwa mjamzito mzito wakati wa kifo chake.

Muhtasari

•Mwili wa kamishna msaidizi wa kaunti ya Kirinyaga Mashariki Jacqueline Waliaula ulipatikana nyumbani kwake Jumatano asubuhi. 

•Kamishna wa kaunti ya Kirinyaga Moses Ivuto alisema Idara ya Upelelezi wa Jinai inachunguza tukio hilo. 

Kamishna msaidizi wa kaunti ya Kirinyaga Mashariki Jacqueline Waliaula.
Kamishna msaidizi wa kaunti ya Kirinyaga Mashariki Jacqueline Waliaula.
Image: HISANI

Wapelelezi wa DCI wanachunguza kisa ambapo afisa mmoja wa serikali alipatikana amefariki katika nyumba yake kaunti ya Kirinyaga.

 Mpelelezi mmoja anayehusika na uchunguzi huo aliarifu kwamba mwili wa kamishna msaidizi wa kaunti ya Kirinyaga Mashariki Jacqueline Waliaula ulipatikana nyumbani kwake Jumatano asubuhi. 

"Ripoti ya awali inaeleza kwamba alitapika jana usiku na kusema angeenda hospitali leo," mpelelezi ambaye aliomba hifadhi ya jina kutokana na unyeti wa suala hilo alisema.  

Mpelelezi huyo alisema mwili wa marehemu uligunduliwa chumbani kwake na yaya ambaye baadaye alimjulisha jirani yao ambaye ni afisa wa polisi. 

"Yaya yake aliamka na kuanza kazi yake ya kuandaa kifungua kinywa lakini alishuku kuwa kuna kitu kilikuwa kibaya kwani alikuwa hajatoka chumbani kwake.

Aliamua kwenda chumbani kwake na kumkuta amelala kitandani kwa tumbo.

Akampigia simu jirani yao. afisa wa polisi, na ilikuwa wakati huu ambapo alithibitishwa kuwa amekufa," alisema. 

Kamishna wa kaunti ya Kirinyaga Moses Ivuto alisema Idara ya Upelelezi wa Jinai inachunguza tukio hilo. 

"DCI imechukua mamlaka na inachunguza tukio hilo," Ivuto alisema kupitia simu Alhamisi. 

Alisema uchunguzi wa maiti ulipangwa kufanyika leo (Alhamisi) ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

 "Tunasubiri wataalam wa magonjwa wafanye uchunguzi wa mwili wa marehemu katika Hospitali ya Jamii, Karatina leo.

Ripoti ya postmoterm itatolewa na daktari wa serikali," Ivuto alisema. 

Marehemu alikuwa mjamzito mzito wakati wa kifo chake. 

 Chanzo cha kifo chake bado hakijajulikana. 

Kifo chake kinakuja siku chache baada ya msimamizi mwingine mkuu kufariki chini ya hali kama hiyo. 

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mathira Mashariki Ibrahim Muchangi alianguka ndani ya nyumba yake na kutangazwa kuwa amefariki katika hospitali siku chache zilizopita. 

Kulingana na ripoti ya uchunguzi wa mwili wa Muchangi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Jamii mnamo Julai 25, alifariki kutokana na mshtuko wa moyo.

"Ripoti ya awali iliyotolewa na wataalamu wa magonjwa ilionyesha kuwa Ibrahim Kiarie Muchangi alipatwa na kifo cha ghafla cha moyo kilichosababishwa na kupungua kwa mishipa ya moyo ambayo hutoa damu kwenye moyo na hivyo kuathiri utendaji wake," ripoti ilisema.