Raia wa Misri auawa mtaani Jamhuri alipoenda kudai pesa zake

Marehemu Ayman Alsaid alidungwa kisu mara nane na mshukiwa aliyejaribu pia kujiua kwa kujikata koo.

Muhtasari

• Polisi waliitwa na jirani baada ya kusikia zogo na kupata watu watatu wakiwa na majeraha ya kudungwa kisu.

• Walikimbizwa katika hospitali ya Coptic ambapo Alsaid alifariki akipokea matibabu. Mwenzake alilazwa lakini hali yake ni thabiti.

Crime scene
Crime scene

Raia mmoja wa Misri ambaye alikuwa ameenda kudai  deni lake kutoka kwa jirani yake alifariki baada ya kudungwa kisu mara nane katika mapigano mtaa wa Jamhuri jijini Nairobi.

Marehemu aliyetambulika kama Ayman Alsaid inasemekana alidungwa kisu mara nane na mshukiwa aliyejaribu pia kujiua kwa kujikata koo.

Polisi walioitwa na jirani baada ya kusikia zogo katika ghorofa ya Orange mtaani Jamhuri walipata watu watatu wakiwa na majeraha ya kudungwa kisu.

Polisi walisema Alsaid na mwenzake alienda kwa nyumba ya mshukiwa na kutaka walipwe deni lao.

Kisha alikasirika na kwenda jikoni, akachukua kisu na kumchoma mhasiriwa mara nane huku mwenzake akichomwa kisu kwenye paja kabla ya kujigeuzia kisu hicho mwenyewe.

Watatu hao walikimbizwa katika hospitali ya Coptic ambapo Alsaid alifariki akipokea matibabu. Mwenzake alilazwa lakini hali yake ni thabiti.

Kwingineko,

Polisi wanasaka genge lililovamia nyumba moja eneo la Chumvi kwenye Barabara kuu ya Mombasa huko Machakos na kumuua mfanyikazi wa nyumbani wakati wa wizi huo.

Mfanyikazi huyo wa kike alikuwa peke yake ndani ya nyumba wakati genge hilo lilipovamia na kumnyonga kabla ya kutoroka na bidhaa za nyumbani zenye thamani ya maelfu ya pesa.

Polisi wanasema wamiliki wa nyumba hiyo walikuwa wamemwacha mwanamke huyo peke yake ndani ya nyumba wakati genge hilo lilipovamia Jumatano alasiri. Msako dhidi ya genge unaendelea.