Uhuru anatishia maisha yangu!- Moses Kuria adai

Kuria anadai kuwa maisha yake kwa sasa yamo hatarini.

Muhtasari

•Kuria alimkosoa IG wa polisi kwa kumpa usalama wa ziada mpinzani wake Kimani Wamatangi katika mikutano yake yote ya kisiasa.

•Mbunge huyo hakutoa uthibitisho wowote wa kuthibitisha madai kwamba alikuwa anatishiwa na Rais.

Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Image: MAKTABA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria sasa anadai kuwa Rais Uhuru Kenyatta anatishia maisha yake.

Kuria kupitia taarifa ya kupinga Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alidai kuwa maisha yake yamo hatarini, madai ambayo hayajathibitishwa. 

Mbunge huyo mwenye utata alimkosoa IG wa polisi kwa kumpa usalama wa ziada mgombeaji wa ugavana Kiambu wa UDA Kimani Wamatangi katika mikutano yake yote ya kisiasa.

Ni wakati akitoa kauli hiyo ambapo alidai Rais Uhuru Kenyatta anamtishia.

"Ndugu IG Mutyambai, huku bosi wako Uhuru Kenyatta akiwa na shughuli nyingi za kutishia maisha yangu, unawapa polisi waliovalia sare kwenye magari matatu chini ya uongozi wa OCS kwa mshindani wangu Kimani wa Matangi kwa mikutano yake yote," alisema kupitia taarifa aliyopakia Facebook Jumamosi.

"Ilifanyika Jumatano huko Mungere huko Lari na jana Ngegu, Kiambu Mjini. Hata Gavana James Nyoro hapati kiwango hiki cha usalama. Tutendee sote kwa usawa na zaidi sisi ambao maisha yao yako hatarini baada ya vitisho vya Uhuru Kenyatta."

Kuria hata hivyo, hakufichua ni kwa nini alitishiwa na rais.

Mbunge huyo pia hakutoa uthibitisho wowote wa kuthibitisha madai kwamba alikuwa anatishiwa na Rais.

Kuria anakodolea macho kiti cha ugavana wa Kiambu kwa tikiti ya chama cha CCK kinachomuunga mkono DP William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais.