DPP aagiza uchunguzi wa yanayodaiwa kuwa mazungumzo ya simu ya Junet na afisa wa IEBC

Haji amemwagiza IG Mutyambai kuchunguza Junet anasikika akipanga mkutano na maafisa wa IEBC.

Muhtasari

•DPP Noordin Haji anasema iwapo klipu hiyo itapatikana kuwa ya kweli basi mazungumzo hayo ni sawa na kosa la uchaguzi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
DPP Norrdin Haji Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
Image: Maktaba

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameagiza Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kuchunguza uhalisi wa rekodi ya sauti ambapo anayedaiwa kuwa Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed anasikika akipanga mkutano na maafisa wa IEBC.

DPP Noordin Haji anasema iwapo klipu hiyo itapatikana kuwa ya kweli basi mazungumzo hayo ni sawa na kosa la uchaguzi.

“Matamshi yaliyonaswa kwenye rekodi ya sauti na mkutano unaodaiwa baadae yanaweza kuwa kinyume na kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi ya mwaka 2016 na kifungu cha 15 cha Sheria ya Makosa ya Kompyuta na Makosa ya Mtandao ya mwaka 2018,” alisema Haji katika barua yake kwa Mutyambai.

Katika mazungumzo hayo ya simu yanayodaiwa kuwa kati ya Junet na afisa wa IEBC, mbunge huyo anasikika akipanga mkutano na makamishna wa IEBC wakiwemo mwenyekiti Wafula Chebukati na wengine.

“Sasa kuna kikao cha hali ya juu ulikuwa ukiniuliza...nataka tuuandae kesho saa kumi na mbili jioni, hili jambo tutalijadili na tunatakiwa kulipatia ufumbuzi,” anayedaiwa kuwa Junet amenukuliwa akisema katika klipu hiyo.

"Kuna tatizo hapo...tunatakiwa kulitatua," aliongeza.

Agizo la DPP linafuatia lingine sawia ambapo anamtaka Inspekta Jenerali kubaini uhalisi wa video ambayo Naibu Rais William Ruto anasikika akisema maneno ya chuki dhidi ya baadhi ya jamii katika kaunti ya Uasin Gishu.

Junet na Gavana wa Mombasa Hassan Joho walichapisha video hiyo kwenye kurasa zao za Twitter Jumanne.

Klipu hiyo ilikarabatiwa ili kuonyesha kwamba DP alikuwa akisema maneno ya chuki dhidi ya jamii fulani zinazoishi eneo la bonde la ufa na kutangaza aibu kwao.

"Faili ya uchunguzi inapaswa kuwasilishwa kwa afisi ndani ya siku saba kutoka tarehe yake," Haji alimwambia Mutyambai.