Watu saba wamefariki baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kalama Community Conservancy kando ya barabara kuu ya Isiolo - Moyale.
Kulingana na ripoti za awali zilizotolewa na Naibu OCPD wa Samburu Mashariki, Juma Boy, saba hao waliangamia papo hapo huku wengine saba wakipata majeraha mabaya.
Juma alisema kuwa watu hao 15 walikuwa wakisafiri kuelekea Samburu kusherehekea ushindi wa uchaguzi.
OCPD, hata hivyo, hakufichua mara moja ni ushindi wa nani ambao watu hao saba walikuwa wanaenda kusherehekea.
Majeruhi hao walikimbizwa katika kituo cha afya kilicho karibu kwa matibabu huku wale waliojeruhiwa vibaya wakilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
"Ripoti ya awali inaonyesha wengi wao walikuwa wanatoka eneo la Lorubae ndani ya Archers Post na walipaswa kukutana na mwanasiasa huyo huko Leerata kwa sherehe," Juma alisema.
Taarifa za mashuhuda zilieleza kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi kabla ya kuacha njia na kubingiria mara kadhaa.