Wazazi wanasihi serikali kufutilia mbali karo ya siku za likizo

Wazazi sasa wako na mtazamo tofauti kote nchini kuhusu karo

Muhtasari

•Wanafunzi hao walijazana kwa vituo mbalimbali vya mabasi jijini Nairobi kupata usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali.

 

Waziri wa Elimu George Magoha katika shule moja eneo la Kabete Nairobi
Waziri wa Elimu George Magoha katika shule moja eneo la Kabete Nairobi
Image: HISANI

Wazazi sasa wako na mtazamo tofauti kote nchini wakati huu ambapo wanafunzi wameanza kurudi shuleni, wengi wakiomba  serikali kuwaruhusu kutolipa karo kwa muda ambao wanafunzi walikaa nyumbani.

Katika kaunti ya Homa Bay, wazazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wa masomo ya kidijitali, Julius Omuga wanataka wizara hiyo kurekebisha malipo ya karo kwa muhula huu ili kutojumuisha  siku ambazo  wanafunzi walikuwa nyumbani kwa sababu za uchaguzi mkuu.

"Wazazi wanalemewa na gharama ya juu ya maisha, ambayo inawafanya kushindwa kulipa karo," Omuga alisema.

Katika kaunti ya Kiambu, kulikuwa na idadi ndogo ya wanafunzi ambao walirejea shuleni kuendeleza masomo kutoka pale walipoachia kabla ya kufunga shule kuelekea uchaguzi mkuu. Wazazi wengi walisema kuwa bado wako katika harakati za kutafuta karo.

Wakiongozwa na Lucy Wambui ambaye ni mmoja wa wazazi, waliisihi serikali kutathmini mipango mipya ya tarehe za uchaguzi ikiwa mahakama ya upeo wa juu itabatilisha uamuzi wa IEBC kumkabidhi rais mteule Ruto cheti cha ushindi. kulingana nao, hili litahakikisha muda wa wanafunzi shuleni hauathiriki kwa njia yoyote ile.

“Serikali inapaswa kupanga upya ratiba zake na ikiwezekana ipange uchaguzi mwezi Desemba tukiwa na watoto wetu nyumbani kwa likizo ndefu. Uchaguzi wa mwaka huu ulionekana kutatiza masomo licha ya kuwa kalenda ya kawaida ya masomo bado haijarejea,” alieleza Wambui.

Hata hivyo maelfu ya wanafunzi walirudi shuleni Alhamis baada ya mapumziko ya takriban majuma mawili ya katikati mwa muhula kwasababu ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Wanafunzi hao walifurika katika vituo mbalimbali vya magari ya uchukuzi wa umma jijini kote nchini kupata usafiri kurejea shuleni.