Biwi la simanzi limetanda katika shule ya upili ya Migingo Girls katika kaunti ndogo ya Kadibo baada ya naibu mwalimu mkuu wao kupatikana akiwa amechomwa ndani ya nyumba yake ndani ya boma la shule hiyo.
Mwanawe marehemu Roseline Atieno, Jeff Onyango mwenye umri wa miaka 27 anadaiwa kutekeleza mauji hayo. Onyango alikamatwa baada ya kupatikana ndani ya nyumba na marehemu na kwa sasa anazuiliwa na polisi.
Kulingana na ripoti ya polisi, tukio hilo liliripotiwa Jumapili mwendo wa saa mbili usiku na mtoto wa marehemu Stephen Allan Nyawada.
Allan alikuwa ameenda kumtembelea mama yake shuleni na alipobisha hodi, mlango ulikuwa umefungwa kutoka ndani.
Aliripoti kwamba alisikia mtu akitembea karibu na nyumba na mara kaka yake Jeff Onyango akafungua mlango.
Alipoingia ndani, alikuta mlango wa bafuni umefunguliwa na mama huyo ameungua kiasi cha kutotambulika.
Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Rabuor, maafisa wa DCI na wataalam wa uhalifu walitembelea eneo la tukio na kubaini kuwa marehemu alikuwa akiishi pamoja na mshukiwa ndani ya uwanja wa shule.
"Kulikuwa na masizi ukutani na mafuta ya taa kwenye kikombe mlangoni ikiwa bafuni na kisu cha jikoni kilipatikana kando ya mwili. Na jikoni kulikuwa na taa ya Blizzard na mafuta ya taa ambayo inaaminika kutumika kutekeleza uhalifu,” Afisa mmoja alisema.
Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Star Annext mjini Kisumu ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.