"Natamani ningekuwa kwenye debe" Sonko asema huku akimpongeza Nassir

Sonko amemtambua mbunge huyo wa zamani wa Mvita kama gavana wa pili wa kaunti ya Mombasa.

Muhtasari

• Sonko amempongeza mgombea ugavana wa Mombasa kwa tikiti ya ODM Abdulswamad  Nassir hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa.

•Alidokeza anatamani sana angeruhusiwa kuwania kiti cha ugavana wa kaunti hiyo ya Pwani kama ilivyokuwa azma yake.

Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Image: Facebook//Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amempongeza mgombea ugavana wa Mombasa kwa tikiti ya ODM Abdulswamad Sharrif Nassir hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa kaunti hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Sonko amemtambua mbunge huyo wa zamani wa Mvita kama gavana wa pili wa kaunti  ya Mombasa.

Huku akimpongeza Nassir, Sonko pia aliwashukuru wafuasi wa mgombea wa UDA Hassan Omar Sarai kwa uungaji mkono wao na kwa kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa gavana  uliofanyika Jumatatu.

"Licha ya kupoteza, tuendelee kuwa na nguvu na umoja zaidi kwani tutakuwepo kwa ajili yenu kila mmoja hata wale ambao hawakuwahi kutupigia kura. Nitaendelea kuwaunga mkono nyote katika uwezo wangu mdogo na wa timu yangu ya Sonko Rescue Team. Mungu abariki watu wa Mombasa, Mungu ibariki Kenya," Sonko alisema.

Gavana huyo wa zamani alibainisha kuwa katika kila shindano, mshindani wako sio adui yako bali ni mpinzani wako.

Alidokeza anatamani sana angeruhusiwa kuwania kiti cha ugavana wa kaunti hiyo ya Pwani kama ilivyokuwa azma yake.

"Asiyekubali kushindwa sio mshindani Hongera Abdulswamad Sharrif Nassir kwa ushindi wako kama Gavana wa pili wa Mombasa, tunaishi kupigana siku nyingine," Alisema.

Usiku wa kuamkia Jumanne, sherehe kubwa zilitikisa eneo la biashara la katikati mwa jiji la  Mombasa  baada ya kubainika kuwa  Abdulswamad Nassir alikuwa akiongoza katika vituo vingi vya kupigia kura.

Nassir aliongoza kwa pengo kubwa dhidi ya mpinzani wake mkuu Hassan Omar wa UDA.

Gavana wa Mombasa anayeondoka Hassan Joho na Nassir waliwaongoza wafuasi wa ODM katika kusherehekea kuzunguka mitaa ya Mombasa.

Maelfu ya wafuasi walikusanyika kwenye Treasury Square wakiwa tayari kusherehekea.

Viongozi waliozungumza usiku walikejeli timu ya Kenya Kwanza kwa 'kujipiga kifua' kabla ya siku ya uchaguzi.

Joho alisema urafiki wake na Nassir ulianza muda mrefu kabla ya kujiunga na siasa.

“Tumekuwa ndugu kabla ya siasa, tumekuwa ndugu kwenye siasa na tutaendelea kuwa ndugu baada ya siasa,” alisema.

Joho pia alimpigia simu Raila Odinga ili kuzungumza na umati uliokuwa na furaha.

Raila aliwashukuru wafuasi hao kupitia simu.

“Hongera kwa wakazi wa Mombasa,” Raila alisema.