Kalonzo ajiondoa kwenye kinyang'anyiro cha spika

Kiongozi huyo wa Wiper alikuwa amezimezea mate nyadhifa za spika wa bunge la kitaifa na seneti.

Muhtasari

•Hii ni baada ya kikao cha kitaifa cha chama  cha Wiper kusema azma hiyo itakuwa ya kufedhehesha.

•Wabunge wengi wanaamini kuwa idadi haipendelei muungano wa Azimio- One Kenya ikizingatiwa kwamba baadhi ya wanachama wao wamehamia Kenya Kwanza.

KINARA WA WIPER KALONZO MUSYOKA
Image: WILFRED NYANGARESI

Kiongozi wa Wiper Stephen Kalonzo Musyoka hatawania wadhifa wa spika wa bunge lolote nchini Kenya.

Kulingana na NTV, hatua hiyo ya makamu rais huyo wa zamani ilifuatia baada ya baraza ya chama cha chake cha Wiper kusema kuwa azma hiyo itakuwa ya kufedhehesha.

Jumanne baraza la Wiper lilikutana katika makao makuu ya chama na kumshawishi kiongozi wao kuacha azma yake kuwania uspika na kulenga kujenga jina lake.

Wabunge wengi wanaamini kuwa idadi katika mabunge yote mawili haipendelei muungano wa Azimio- One Kenya ikizingatiwa kwamba baadhi ya wanachama wao wamehamia Kenya Kwanza.

Kiongozi huyo wa Wiper alikuwa amechukua stakabadhi za kutafuta nyadhifa za spika wa Bunge la Kitaifa na seneti.

Katika Seneti, Kalonzo alikuwa miongoni mwa watu 15 ambao walikuwa wamechukua karatasi za uteuzi kwa nafasi ya spika na wawili kwa nafasi ya naibu spika.

Watu wengine ambao wamechukua karatasi hizo kufikia sasa ni Isaac Aluoch, Jared Oundo, George Bush, Dkt Rodgers Manana, Beatrice Kinyua, Dorothy Kemunto na Jecinta Lesiangiki.

Josephat Mutua, Mohamud Halake, Michael Gichuri na Joshua Boit pia walichukuwa karatasi za uteuzi katika Bunge.

Kwa nafasi ya naibu spika, Maseneta wateule Karungo wa Thangwa (Kiambu) na Kathuri Murungi (Meru) walikuwa wamechukua karatasi.

Hata hivyo, kinyang'anyiro hicho kitajulikana baada ya kujua ni nani kati yao atakuwa amerudisha karatasi kufikia Jumatano, saa nane alasiri.

Karatasi za uteuzi zitakazorejeshwa pia zitachunguzwa ili kuhakikisha kuwa wagombeaji wanaafikia vigezo vya sheria.

Maseneta wateule watamchagua spika mara baada ya kuapishwa siku ya Alhamisi.

Miungano yote miwili inapanga vikao vya vikundi vya bunge siku ya Alhamisi wakati bunge la kumi na tatu litafunguliwa.

Baada ya wajumbe wa mabunge yote mawili kuapishwa, utaratibu wa kwanza wa biashara utakuwa ni kuchagua maspika.