Uhuru akutana na Ruto katika Ikulu ya Nairobi kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu kufanyika

Mkutano wa Jumatatu ni wa kwanza kwa Uhuru na Ruto kukutana baada ya miezi kadhaa.

Muhtasari

• Mkutano wa Jumatatu unaonekana kama kikao cha kutuliza hali kabla ya hafla ya ubadilishanaji wa mamlaka wakati wa kuapishwa kwa Ruto kama Rais wa tano wa Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta wakiwakaribisha Rais Mteule William Ruto na Mkewe Rais mteule Rachel Ruto katika Ikulu Jumatatu, Septemba 12, 2022. Picha: KWA HISANI
Rais Uhuru Kenyatta na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta wakiwakaribisha Rais Mteule William Ruto na Mkewe Rais mteule Rachel Ruto katika Ikulu Jumatatu, Septemba 12, 2022. Picha: KWA HISANI

Rais mteule William Ruto anakutana na Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta katika Ikulu, Nairobi.

Ruto ameandamana na Mkewe Rachel Ruto.

Ripoti ziliarifu kwamba viongozi hao wawili wanafanya mkutano huku Uhuru akimkabidhi Ruto mamlaka katika kiwango cha kibinafsi kabla ya kuapishwa kwa Ruto siku Jumanne katika uwanja wa Kasarani na kukabidhiwa mamlaka rasmi.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kuhutubia taifa katika mkutano wa pamoja na wanahabari baada ya mkutano huo wa faragha ulioanza muda mfupi baada ya saa tisa alasiri.

Mkutano wa Jumatatu unaonekana kama kikao cha kutuliza hali kabla ya hafla ya ubadilishanaji wa mamlaka wakati wa kuapishwa kwa Ruto kama Rais wa tano wa Kenya.

Viongozi hao wawili wamekuwa na uhusiano mbaya kwa miezi kadhaa tangu walipotofautiana kuhusu siasa za urithi.

Uhuru alimuidhinisha kiongozi wa Azimio Raila Odinga ambaye alishindwa na Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mkutano wa Jumatatu ni wa kwanza kwa Uhuru na Ruto kukutana baada ya miezi kadhaa.

Alipokuwa akitoa hotuba yake muda mfupi baada ya uamuzi wa Mahakama ya Upeo mnamo Septemba 5, Ruto alifichua kuwa hakuwa amezungumza na aliyekuwa mshirika wake wa kisiasa kwa miezi kadhaa.