Wajackoyah amjengea marehemu babake nyumba ya vioo baada ya 'kupatana' naye

Marehemu Jakoya alifariki mnamo Desemba 21, 2021 akiwa na umri wa miaka 86.

Muhtasari

•Wajackoyah alionyesha nyumba ya zamani ya marehemu Tito Jakoya Odhiambo na ile mpya iliyopanuliwa na kuboreshwa kwa vioo.

•Pia alionyesha kaburi la marehemu baba yake lililo nje kidogo ya nyumba hiyo ambalo pia aliifanyia ukarabati kwa marumaru.

Image: FACEBOOK// GEORGE LUCHIRI WAJACKOYAH

Mgombea urais wa Roots Party katika kinyang'anyiro cha Agosti 9  George Wajackoyah amemaliza kukarabati nyumba ya marehemu babake.

Siku ya Ijumaa Wajackoyah alionyesha nyumba ya zamani ya marehemu Tito Jakoya Odhiambo na ile mpya iliyopanuliwa na kuboreshwa kwa vioo.

Mwanasiasa huyo ambaye aliibuka wa tatu katika kinyang’anyiro cha urais alisema hatua hiyo ilifuatia maridhiano yake na babake.

"Tunafurahi kutimiza ndoto yetu. Baada ya maridhiano na marehemu baba yangu niliamua kumheshimu kwa mahali pa kupumzika pa marumaru na kumaliza nyumba yake ya kioo," alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Pia alionyesha kaburi la marehemu baba yake lililo nje kidogo ya nyumba hiyo ambalo pia aliifanyia ukarabati kwa marumaru.

Marehemu Jakoya alifariki mnamo Desemba 21, 2021 akiwa na umri wa miaka 86.

Hii ilikuwa miezi michache tu kabla ya Wajackoyah kutangaza azma yake kuwania urais wa Kenya katika uchaguzi wa mwaka huu.

Wakili huyo aliidhinishwa kuwania kiti hicho cha juu zaidi mapema mwezi Juni baada ya kutimiza matakwa ya IEBC.

"Sasa tunaweza kuthibitisha kwamba umetimiza mahitaji ya chini kabisa...tumekubali uteuzi wako kama mgombeaji Urais kwa Uchaguzi Mkuu wa 2022...hongera," Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimwambia mnamo Juni 2.

Wajackoyah aliibuka wa tatu katika kinyang’anyiro hicho ambacho kilishindwa na mgombea wa UDA William Ruto.

Alifanikiwa kupata kura 61,969 (0.44%)  huku Ruto akipata kura 7,176,141 (50.49%.  Mgombea wa Azimio One Kenya Raila Odinga ambaye aliibuka wa pili alipata kura 6,942,930 (48.85).

Waihiga Mwaure wa Chama cha Agano alishikilia nafasi ya mwisho kwa kura 31,987 (0.23).