Rais William Ruto aelekea Uingereza kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II

Ruto aliondoka nchini Jumapili alasiri akiwa ameandamana na mkewe Rachel Ruto.

Muhtasari

•Ruto ni miongoni mwa viongozi 500 wa kigeni watakaohudhuria Mazishi ya Serikali ya Malkia Elizabeth II siku ya Jumatatu.

•Baadae rais ataondoka Uingereza  kuelekea Marekani ambako atahudhuria Mkutano Mkuu wa 77 wa Umoja wa Mataifa (UNGA)

Image: TWITTER//WILLIAM SAMOEI RUTO

Rais William Ruto ameondoka nchini kuelekea katika jiji la London, Uingereza ambako atahudhuria mazishi ya Malkia Elizbeth II.

Ruto ni miongoni mwa viongozi 500 wa kigeni watakaohudhuria Mazishi ya Serikali ya Malkia Elizabeth II siku ya Jumatatu.

Rais aliondoka nchini Jumapili alasiri akiwa  ameandamana na mkewe Rachel Ruto.

Kuimarisha uhusiano na jumuiya ya kimataifa kutachochea mageuzi ya nchi yetu. Niliondoka kwenda London, Uingereza kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II," Ruto alitangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Naibu rais Rigathi Gachagua na katibu mkuu katika wizara ya masuala ya kigeni Amb Macharia Kamau ni miongoni mwa viongozi walikuwepo kumuaga rais kwaheri.

Baada ya kuhudhuria mazishi ya Malkia, rais Ruto ataondoka Uingereza  kuelekea Marekani ambako atahudhuria Mkutano Mkuu wa 77 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) huko mjini New York.

Anatarajiwa kukutana na Rais Joe Biden na maafisa kutoka chumba cha biashara cha Amerika.

Mkutano wa UNGA utakuwa wa kwanza kufanyika ana kwa ana tangu kuanza kwa janga la Covid-19 ambalo lilisitisha kutangamana.

Mikutano ya UNGA mnamo 2020 na 2021 ilifanyikakwa njia ya Kielektroniki.