Jinsi Rigathi alivyofanya mazoezi ya Mdahalo wa Naibu Rais ili kushindana na Karua yafichuliwa

Itumbi alisema muungano wa Kenya Kwanza ulimakinika kuhusu kila hatua wakati wa kampeni.

Muhtasari

•Rigathi alifanya mazoezi mengi kabla ya kuhudhuria mdahalo wa naibu rais ambao ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Katoliki  cha Afrika Mashariki jijini Nairobi  mnamo Julai 19, 2022.

•Itumbi alifichua kuwa pia walifanya mazoezi makali na rais Ruto alipokuwa akijiandaa kwa Mjadala wa Urais ambao ulifanyika Julai 26.

Image: TWITTER// DENNIS ITUMBI

Naibu rais wa Rais Rigathi Gachagua alifanya mazoezi mengi kabla ya kuhudhuria mdahalo wa naibu rais ambao ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Katoliki  cha Afrika Mashariki jijini Nairobi  mnamo Julai 19, 2022 , mtaalamu wa masuala ya kidijitali wa  rais William Ruto Dennis Itumbi amefichua.

Katika taarifa ya Jumanne jioni Itumbi alisema muungano wa Kenya Kwanza ulimakinika kuhusu kila hatua wakati wa kampeni.

"Hustler Nation walifanya kazi kwa bidii. Katikati ya msimu wa kampeni, tulifanya mazoezi kwa midahalo. Hakuna kilichochukuliwa kuwa cha kawaida," Itumbi alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Alifichua kwamba walipokuwa wakifanya mazoezi walifanya mwanamke mmoja kucheza nafasi ya mpinzani wa Rigathi katika mdahalo huo, Martha Karua wa Azimio-One Kenya  ili kuwa na matokeo bora.

"Alifanya kazi yake vizuri, hata alienda bila viatu-kihalisi," alisema Itumbi.

Itumbi alifichua kuwa pia walifanya mazoezi makali na rais Ruto alipokuwa akijiandaa kwa Mjadala wa Urais ambao ulifanyika Julai 26.

Takriban miezi miwili iliyopita Rigathi aliwashangaza Wakenya wengi kwa jinsi alivyofanya katika Mdahalo wa Urais. 

Wakati wa Mdahalo huo mgombea mwenza huyo wa urais wa Ruto  ambaye hatimaye aliibuka kuwa Naibu Rais aliulizwa maswali magumu ambayo alionekana kuwa na majibu yake. Pia aliweza kueleza manifesto ya muungano wa Kenya Kwanza kwa ufasaha alipoulizwa kufanya hivyo.

Baada ya mdahalo huo naibu rais alipongezwa na wanamitandao  Wakenya  ambao wengi wao walionekana kushangazwa na jinsi alivyojiendeleza dhidi ya mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua.

Baadhi ya wanamitandao hata hivyo walimkosoa na kumkejeli kuhusu jinsi alivyojibu baadhi ya maswali aliyoulizwa.