Miguna hatimaye kurejea Kenya baada ya kupokea pasipoti kutoka kwa Ruto

Wakili huyo alidokeza kuwa atarejea pindi tu baada ya vikwazo vinavyomzuia kuingia tena nchini kuondolewa.

Muhtasari

•Jumanne wakili huyo ambaye kwa sasa anaishi Kanada alitangaza kwamba ameweza kupokea pasipoti yake ya Kenya kwa maandalizi ya kurejea.

•Miguna alifukuzwa nchini kwa mara ya kwanza mnamo Februari 6, 2018 baada ya kukamatwa na kuzuiliwa.

Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Image: MAKTABA

Miguna Miguna sasa anaweza kutabasamu kwani kurejea kwake katika nchi yake ya kuzaliwa sasa kunaonekana kukaribia zaidi kuliko hapo awali.

Jumanne wakili huyo ambaye kwa sasa anaishi Kanada alitangaza kwamba ameweza kupokea pasipoti yake ya Kenya kwa maandalizi ya kurejea.

Alibainisha kuwa aliweza stakabadhi hiyo muhimu iliweza kufikishwa kwake  kufuatia agizo la Rais William Ruto.

"Siku 1687 baada ya Uhuru Kenyatta, Raila Odinga, Fred Matiang'i, Karanja kibicho na Jenerali Kihalangwa kupanga njama ya kuchukua na kuharibu Pasipoti yangu ya Kenya kinyume cha sheria, Rais William Ruto amefanya niletewe mpya," Miguna alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mshauri huyo wa kisiasa wa zamani wa aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga alidokeza kuwa atarejea nchini pindi tu baada ya vikwazo vilivyomzuia kuingia tena hapa nchini kuondolewa.

Miguna alifukuzwa nchini kwa mara ya kwanza mnamo Februari 6, 2018 baada ya kukamatwa na kuzuiliwa.Hii ni baada ya kuchukua hatua hatari ya kumuapisha Raila kuwa 'Rais wa Watu' kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Alitakiwa kurejea nchini mwezi Novemba 2021 lakini hakuweza kutokana na vikwazo ambavyo viliwekwa dhidi yake.

Wakili huyo amekuw akiwalaumu  rais wa zamani Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwa masaibu yaliyokumba azma yake ya kurejea nchini.

Hapo awali alidokeza kuwa yupo tayari kurejea baada ya Ruto kutangazwa mshindi wa kinyang'anyiro cha urais.