Mtaala wa CBC hautakomeshwa, DP Gachagua asema

Gachagua alisema badala yake wanaipitia ili waweze kuhifadhi yale yaliyo mema na kuyaboresha.

Muhtasari
  • Alibainisha zaidi kwamba serikali imejitolea kwa uchumi wa ubunifu na maendeleo ya vijana kuwa viongozi wa kesho
Naibu rais mteule Rigathi Gachagua
Naibu rais mteule Rigathi Gachagua
Image: MAKTABA

Naibu Rais Gachagua Rigathi amesema serikali haitabatilisha Mtaala Unaozingatia Umahiri.

Gachagua alisema badala yake wanaipitia ili waweze kuhifadhi yale yaliyo mema na kuyaboresha.

Alisema kumekuwa na mashaka kutoka kwa walimu, wazazi na wadau wengine kwenye CBC na hivyo kutaka kuangaliwa upya.

“Serikali yetu hivi karibuni itazindua kikosi kazi kitakachoangalia mageuzi ya kielimu ikiwamo CBC kwa nia ya kuipitia na si kuifuta,” alisema.

Alizungumza wakati wa kufungwa kwa Tamasha la 94 la Muziki la Kenya katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu.

DP pia alichukua fursa hiyo kuwaomba Wakenya kushiriki katika mchakato huo mara tu utakapoanza.

“Msilalamike tu kwenye nyumba zenu au sokoni, vituoni, jitokezeni kwa wingi na toeni maoni yenu kuhusu kile mnachotaka kiboreshwe,” alisema.

Alibainisha zaidi kwamba serikali imejitolea kwa uchumi wa ubunifu na maendeleo ya vijana kuwa viongozi wa kesho.

“Serikali yetu imejizatiti kutoa sera na mipango madhubuti ili kuhakikisha kuwa vipaji vya vijana wetu vinatafsiriwa kuwa chanzo cha mapato kwao,” alisema.