Wanane wafariki baada ya matatu kugongana na tangi la mafuta Homa Bay

Ajali hiyo ilitokea baada ya matatu ya abiria kugongana ana kwa ana na lori la mafuta Jumatatu jioni.

Muhtasari
  • Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Homa-Bay alisema abiria wawili waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa-Bay
  • Ajali hiyo ilitokea baada ya matatu ya abiria kugongana ana kwa ana na lori la mafuta Jumatatu jioni
Ajali
Ajali
Image: HISANI

Watu wanane walifariki na wengine wawili kujeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani eneo la Ngengu kando ya barabara ya Homa Bay - Kendu Bay.

Ajali hiyo ilitokea baada ya matatu ya abiria kugongana ana kwa ana na lori la mafuta Jumatatu jioni.

Kamanda wa Polisi wa Homa Bay Samson Ole Kinne alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kubainisha kuwa marehemu alifariki dunia papo hapo.

Mvulana wa darasa la Saba kutoka shule ya Janeiro Junior Academy katika eneo bunge la Rangwe ambaye alikuwa akisafiri kurudi shuleni ni miongoni mwa abiria wanane waliothibitishwa kufariki.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Homa-Bay alisema abiria wawili waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa-Bay huku miili ya marehemu ikipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti ndani ya kituo kimoja.

Uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo.