Uteuzi wa ODM katika bunge la Nairobi wapingwa mahakamani

Walalamishi wanadai kuwa wao ndio watu sahihi kuteuliwa.

Muhtasari

•Wanne hao wameomba mahakama itoe amri ya kumzuia karani wa bunge la kaunti kusimamia uapisho wa Jeckonia Junga Onyango na Nasra Harilal Nanda.

•Kulingana na karatasi za mahakama, walalamishi hao wanadai kuwa walihitimu kuingia kwenye orodha ya uteuzi wa ODM.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Hisani

Watu wanne wamewasilisha kesi mahakamani kupinga orodha ya uteuzi wa ODM katika bunge la kaunti ya Nairobi.

Eric Holi, Night Meda Kazungu, Mirriam Wamboi Nekesa na Brian Shemu Owino wameomba mahakama itoe amri ya kumzuia karani wa bunge la kaunti kusimamia uapisho wa Jeckonia Junga Onyango na Nasra Harilal Nanda.

Pia wanataka mahakama itoe amri ya kusimamisha orodha ya wateule kusubiri uamuzi wa kesi iliyoko mahakamani.

Holi ni mlemavu ilhali Kazungu anatoka kabila la Giriama, ambalo ni jamii ya watu waliotengwa jijini Nairobi, na Nekesa ni kijana. Wanadai kuwa wao ndio watu sahihi kuteuliwa.

"Tunaamini kuwa uteuzi wa wanachama wa bunge la kaunti chini ya Kifungu cha 177 cha Katiba haufai kuegemezwa kwa upendeleo bali mahitaji ya watu wenye ulemavu, vijana na jamii zilizotengwa," karatasi za korti zilisoma.

Walisema wateule hao wawili hawaridhishi kiwango cha kikatiba kilichowekwa chini ya Kifungu cha 177 kwa vile hawatoki katika makundi ambayo yanaweza kuchukuliwa kuwa yametengwa jijini Nairobi.

"Ni muhimu kutoa amri za muda ili kuzuia wahojiwa dhidi ya kukiuka haki za [watu wenye ulemavu], vijana na waliotengwa," walisema katika karatasi za mahakama.

Kulingana na karatasi za mahakama, walalamishi hao wanadai kuwa wameingia kwenye orodha ya uteuzi wa ODM.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka iliendelea kuchapisha orodha iliyopewa jina ‘wajumbe walioteuliwa wa mabunge ya kaunti’ mnamo Septemba 9 mwaka huu.

Watu waliotajwa kama waliopendekezwa katika orodha hiyo ni Onyango na Nanda. Wote wawili waliteuliwa chini ya kitengo kinachoelezewa kama kabila.

Jaji Mugure Thande aliagiza kwamba hati hizo ziwasilishwe kwa ODM, IEBC na spika wa bunge la kaunti ya Nairobi.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 5 kwa maelekezo zaidi.