logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Serikali ya Uganda yajitenga na matamshi ya mwanawe Museveni kuhusu Kenya

Uganda imesisitiza kuwa nchi hiyo jirani inathamini uhusiano mzuri uliopo kati yake na Kenya.

image
na Samuel Maina

Habari04 October 2022 - 12:01

Muhtasari


  • •Muhoozi ambaye ni Kamanda wa Majeshi wa nchi kavu ya Uganda alichapisha msururu wa jumbe tatanishi kwenye Twitter  zilizoonekana kudhalilisha nchi ya Kenya na katiba yake.
KWA HISANI

Serikali ya nchi jirani Uganda imejitenga  mbali na matamshi ya mwanawe rais Museveni, Muhoozi Kainerugaba, yaliyolenga Kenya. 

Jumatatu jioni na Jumanne asubuhi, Muhoozi ambaye ni Kamanda wa Majeshi wa nchi kavu ya Uganda alichapisha msururu wa jumbe tatanishi kwenye Twitter  zilizoonekana kudhalilisha nchi ya Kenya na katiba yake.

Hata hivyo,Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imesisitiza kuwa nchi hiyo jirani inathamini uhusiano mzuri uliopo kati yake na Kenya.

"Wizara ya Mambo ya Nje inapenda kufafanua kwamba serikali ya jamhuri ya Uganda haifanyi Sera yake ya kigeni na shughuli nyingine rasmi kupitia mitandao ya kijamii wala haitegemei vyanzo vya mitandao ya kijamii katika kushughulika na serikali nyingine huru," taarifa iliyotolewa Jumanne ilisoma.

"Kwa hivyo, serikali ya Jamhuri ya Uganda, inapenda kusisitiza uhusiano wake mzuri na jamhuri ya Kenya na kuwahakikishia watu na serikali ya Jamhuri ya Kenya kuhusu uhusiano wetu mzuri tunaouthamini."

Katika ujumbe wake wa kwanza Jumatatu, Muhoozi alimtaja aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kama “kakake mkubwa’ na kumlaumu kwa kutowania urais kwa muhula wa tatu, na kuongeza kuwa angeshinda uchaguzi kwa urahisi.

"Tatizo langu pekee na kaka yangu mkubwa ni kwamba hakugombea muhula wa tatu. Tungeshinda kirahisi," aliandika.

Mwanawe Museveni alizidi kuidhalilisha Katiba ya Kenya akisema Uhuru alipaswa kubadilisha katiba ili kusalia madarakani.

"Haha! Nawapenda jamaa zangu wa Kenya. Katiba? Utawala wa sheria? Lazima uwe unatania! Kwetu (Uganda), kuna Mapinduzi tu na muda si mrefu mtayafahamu!" alisema.

Muhoozi aliendelea kudai kwamba itamchukua yeye na jeshi lake chini ya wiki mbili kuchukua udhibiti wa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

"Haingetuchukua sisi, jeshi langu na mimi, wiki 2 kuteka Nairobi," alisema.

Wakenya waliokuwa wamejawa na ghadhabu walikita kambi kwenye akaunti ya Twitter ya Muhoozi na kujibu matamshi yake.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved