Rais William Ruto leo Jumanne atakagua mradi wa Kings Serenity Affordable Housing Programme, ambao unalenga kujenga ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika mtaa wa Ongata Rongai.
Mradi huo ni wa aina yake huko Rongai. Nyumba hizo ni za vyumba viwili vya kulala.
Nyumba hizo ambazo zimejengwa katika mandhari tulivu ni moja wapo wa miradi ya Boma Yangu ambao ajenda yake kuu ni kutoa nyumba za bei nafuu kwa Wakenya wa mapato ya chini.
Mapema mwezi huu, Ruto alisema Serikali itaboresha mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ili kuwezesha watu wa mapato ya chini kumiliki nyumba.
Kiongozi huyo wa taifa alisema atashirikiana na wabunge kutafuta njia mwafaka zaidi ya kufanikisha mpango wa nyumba za bei nafuu.
Alipokuwa akikagua mradi unaoendelea wa nyumba za bei nafuu mjini Nairobi, Ruto alitangaza kuwa serikali yake itaanzisha nyumba 500,000 za bei nafuu kote nchini.