Kamati ya Bunge ya Uteuzi imekataa kwa kauli moja pendekezo la rais William Ruto kumteua Peninah Malonza kuwa waziri wa Utalii, Wanyamapori na Turathi za kitaifa.
Katika notisi ya hoja hiyo, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichungwah alisema Kamati inayoongozwa na Spika Moses Wetang'ula iliidhinisha uteuzi wa wateule wengine 21 wa Baraza la Mawaziri.
Kamati hiyo pia iliidhinisha uteuzi wa Justin Muturi kama Mwanasheria Mkuu na Mercy Wanjau kama Katibu wa Baraza la Mawaziri.
Kiranja wa walio wachache Junet Mohamed, hata hivyo, alisema upande wa wachache umeandika ripoti yao kukataa uteuzi wa Aisha Jumwa na Mithika Linturi.
Rais William Ruto alimpendekeza Jumwa kuwa waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia na Linturi kwa wizara ya Kilimo na ustawi wa Mifugo.