Rais William Ruto ataongoza shughuli ya kuaga kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Kenya - KDF kinachoelekea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - DRC ambapo mapigano makali yanaendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa M23.
Jeshi la DRC pia linajishughulisha na pande nyingine zinazopigana na kundi la Islamic State - Allied Democratic Forces ADF, na makundi mengine kadhaa yenye silaha.
Vikosi vya Kenya vitajiunga na kikosi cha kanda kitakachosaidia kupambana na makundi yenye silaha.
Wazo la kutuma jeshi la kikanda lilitolewa na kuidhinishwa mwezi Juni, wakati Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta (sasa mjumbe wa amani wa Kenya) alipoitisha mkutano wa amani (Mchakato wa Nairobi) wa viongozi wa EAC.
Kenya ilichaguliwa kuongoza juhudi za kidiplomasia na kijeshi.
Hii ni mara ya kwanza kwa EAC kutuma wanajeshi katika nchi wanachama. Itakuwa mtihani mdogo wa uwezo wa kambi hiyo kushughulikia changamoto tata za kisiasa na usalama.
Kikosi cha Kenya ambacho kilipelekwa mwaka jana kujiunga na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC - MONUSC kwa mwaliko wa Rais Felix Tshisekedi tangu wakati huo kiondolewa na kurejeshwa nyumbani Kenya.