Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Narok Kaskazini Frederick Shiundu amekashifu kisa ambapo wananchi walimshambulia mwanamke asiye na akili timamu kwa madai ya kuiba watoto katika eneo la Motonyi.
Shiundu alisema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna mwanamke aliyekuwa akiiba watoto wadogo katika eneo hilo na wananchi wakaamua kumuadhibu kwa kumpa kichapo cha mbwa.
Bosi huyo wa polisi alisema walikimbia katika eneo hilo kumuokoa mwanamke huyo aliyekuwa amefungwa kamba miguuni na kujeruhiwa vibaya mwili mzima.
Alisema walimuokoa mara moja na kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok kwa matibabu ambapo alithibitishwa kuwa mlemavu wa akili.
“Mwanamke huyo bado amelazwa hospitalini akiwa na majeraha mengi mwilini mwake. Taarifa za hospitali zinaonyesha amekuwa akiishi na ugonjwa wa akili,” alisema.
Shiundu alisema hakuna tukio la kupotea kwa mtoto ambalo limeripotiwa katika kata kaunti nzima na kushangaa ni wapi wakazi hao walikozipata taarifa hizo.
Alisema polisi wanachunguza suala hilo ili kuwakamata waliohusika katika tukio hilo la kusikitisha akiwaonya wakazi dhidi ya kuchukua sheria mkononi.
“Nataka kuwakumbusha wakazi kuwa ni vibaya kujichukulia sheria mkononi. Ukishuku mtu anafanya biashara haramu, unapaswa kuripoti kwa polisi mara moja ili uchunguzi ufanywe,” alisema.
Klipu ya video ya mwanamke huyo akipigwa na wakazi ilikuwa imesambaa kwenye mitandao wa kijamii ambapo alidaiwa alishirikiana na watu wengine wasiojulikana kuiba watoto.