Mpango wa Kazi Mtaani utageuzwa kuwa mpango wa upandaji miti, Rais Ruto atangaza

"Tunapaswa kuanzisha shughuli za muda mrefu za kukabiliana na ukame na ukosefu wa chakula," alisema.

Muhtasari
  • Mkuu wa Nchi alisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko yatabia nchi ambayo Kenya inakabiliana nayo
RAIS WILLIAM RUTO
Image: TWITTER

Mpango wa Kazi Mtaani utabadilishwa kuwa mpango wa upandaji miti, Rais William Ruto ametangaza.

Mkuu wa Nchi alisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko yatabia nchi ambayo Kenya inakabiliana nayo.

"Tunapaswa kuanzisha shughuli za muda mrefu za kukabiliana na ukame na ukosefu wa chakula," alisema.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi siku ya Ijumaa alipobadilishana mawazo na jumuiya ya wafanyabiashara na washirika wa maendeleo kuhusu hali ya ukame nchini Kenya, Rais aliongeza kuwa vijana badala yake watajishughulisha na kazi za ujenzi katika vituo vikuu vya mijini kote nchini.

Rais alisema hali bado ni mbaya haswa katika kaunti 20 kutokana na kuharibika kwa mazao kutokana na mvua kushindwa kunyesha.

Rais Ruto leo alieleza kuwa mradi wa Kazi Mtaani ulioanzishwa na utawala wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ulikuwa na mapato ya chini na fursa finyu kwa vijana ikilinganishwa na shughuli yake ya upandaji miti, ambayo ingeongeza idadi ya vijana.