Waziri wa elimu Machogu afafanua nyongeza ya karo kwa shule za upili

"Mtu yeyote anayesema idadi hiyo imebadilishwa, huyo hayuko hapa Kenya.

Muhtasari
  • Hii ni baada ya waraka uliotumwa kwa maafisa wakuu wa elimu kuashiria mabadiliko ya karo za shule
EZEKIEL MACHOGU
Image: EZEKIEL AMING'A

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amefafanua hatua ya serikali kufutilia mbali ruzuku ya karo za shule za upili.

Machogu alipokuwa akizungumza katika shule ya upili ya Wajir siku ya Jumatano alisema hatua hiyo ilisababishwa na kurejea kwa hali ya kawaida katika kalenda ya shule.

“Kuanzia Januari 23, tutakuwa na mihula mitatu kama ilivyokuwa awali hivyo muundo wa ada unabaki kuwa ule ule wa miaka miwili iliyopita,” Machogu alisema.

Hii ni baada ya waraka uliotumwa kwa maafisa wakuu wa elimu kuashiria mabadiliko ya karo za shule.

"Mtu yeyote anayesema idadi hiyo imebadilishwa, huyo hayuko hapa Kenya. Kubadilisha ada ya shule kutahitaji kikosi kazi nyingine," alisema.

Kwa sababu ya kalenda ya shule iliyobanwa ambayo ilisababishwa na Covid-19, wizara ilipunguza ada kwa Sh8,500.

Kulingana na waraka kutoka kwa wizara hiyo, wazazi watalazimika kulipa Sh53,554 kwa shule za kitaifa, kama ilivyokuwa kabla ya kupunguzwa.

Hii itatumika kwa shule za kitaifa na za ziada za kaunti katika kaunti saba.