Afisa wa polisi aliyekuwa akikabili washukiwa wa ujambazi kufunguliwa mashtaka ya mauaji

Ahmed Rashid, anadaiwa kuongoza kitengo cha polisi 'Pangani Six',kilichokuwa kinawakabili vilivyo majambazi sugu.

Muhtasari

• IPOA ilisema kuwa uchunguzi wake ulibaini kwamba vifo vya Jamal Mohamed na Mohamed Dahir Kheri vilisababishwa na polisi.

Ahmed Rashid afisa wa polisi aliyejulikana kwa kukabiliana na majambazi mtaani Eastleigh.
Ahmed Rashid afisa wa polisi aliyejulikana kwa kukabiliana na majambazi mtaani Eastleigh.
Image: HISANI

Afisa wa polisi aliyeonekana kwenye video mnamo Machi 2017 akiwafyatulia risasi washukiwa wawili wa ujambazi mtaani Eastleigh, sasa anakabiliwa na shtaka la mauaji.

Ahmed Rashid, anadaiwa kuongoza kitengo maalum cha polisi 'Pangani Six',kilichokuwa kinawakabili vilivyo majambazi sugu katika maeneo ya Eastleigh na Mathare.

Maafisa hao hata hivyo walihusishwa na mauaji kadhaa ya kiholela.

Rashid anatarajiwa kufikishwa mahakamani Desemba 8, 2022 kukubali au kukanusha mashtaka baada ya Mamlaka Huru ya Kusimamia shughuli za Polisi (IPOA) kupokea agizo la kumuita Mahakamani.  

"Mamlaka Huru ya Kusimamia shughuli za Polisi ilikamilisha uchunguzi wa vifo vya Jamal Mohamed na Mohamed Dahir Kheri kufuatia kisa cha ufyatulianaji wa risasi mtaani Easteigh, Kaunti ya Nairobi mnamo Machi 31, 2017 na kubaini kuwa vifo hivyo vilisababishwa na kitendo cha polisi," Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori alisema katika taarifa yake.

"Kwa kuongozwa na Kifungu cha 29(a) cha Sheria ya IPOA, matokeo ya uchunguzi yalipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na mapendekezo ya kumfungulia mashtaka Ahmed Rashid, kwa mauaji."

Bi Makori aliongeza kuwa mamlaka hiyo imekusanya ushahidi wa kutosha kumshtaki Rashid kwa mauaji baada ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vifo vya watu waliotajwa.

Katika mahojiano na BBC Africa kuhusiana na mauaji ya washukiwa hao wawili, Rashid alidaiwa kukiri kuwaua wawili hao.