Aliyekuwa OCS wa Pangani atiwa mbaroni,kwa madai ya kuwadhulumu maafisa wa kike

Hata aliandaa hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wa kike ambao walishindwa kushirikiana naye.

Muhtasari
  • Kulingana na ripoti ya uchunguzi, mmoja wa walalamishi aliripoti kwamba alivamiwa na kushambuliwa kingono na Samir
Pingu
Image: Radio Jambo

Aliyekuwa OCS wa Kamukunji na Pangani, Inspekta Mkuu Samir Yunis, alikamatwa Jumatatu kwa tuhuma za kutumia wadhifa wake kuwadhulumu wafanyakazi wenzake wa kike.

Samir anatarajiwa kushtakiwa mahakamani Jumatano, Desemba 7, na makosa kadhaa ya matumizi mabaya ya nafasi ya mamlaka kinyume na kifungu cha 24(2)(a) cha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, 2006.

Kifungu cha 24 (2) cha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana kinasema mtu yeyote ambaye ni afisa wa kutekeleza sheria anachukua nafasi yake na anafanya ngono au anatenda kosa lingine lolote la kujamiiana ndani ya mipaka ya kituo alichopangiwa, anatenda kosa la matumizi mabaya ya nafasi ya mamlaka na akitiwa hatiani atawajibika kwa kifungo kisichopungua miaka 10.

Samir alikamatwa Jumatatu na maafisa wa upelelezi kutoka Kitengo cha Masuala ya Ndani (IAU) baada ya kuheshimu wito wa kufika mbele ya mkurugenzi wa IAU.

Alizuiliwa kwa muda katika Kituo cha Polisi cha Capitol Hill ambapo alama zake za vidole zilichukuliwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana ya Sh10,000 pesa taslimu.

IAU ilianzisha uchunguzi kuhusu mienendo ya Samir, ambaye alihudumu katika vituo vya Dandora, Kamkunji, Mombasa Central na Pangani kufuatia malalamishi kadhaa ya maafisa wa kike.

“Maafisa hao waliandika malalamishi kadhaa kwa Inspekta Jenerali na IPOA wakidai kuwa afisa huyo alikuwa akitumia nafasi yake kama OCS kuwalazimisha kufanya naye mapenzi. Waliokataa walikuwa wakinyanyaswa na kuhamishwa bila kufuata taratibu za kawaida,” IAU ilisema.

Hata aliandaa hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wa kike ambao walishindwa kushirikiana naye.

Kulingana na ripoti ya uchunguzi, mmoja wa walalamishi aliripoti kwamba alivamiwa na kushambuliwa kingono na Samir..

Hata hivyo, licha ya kuwasilisha malalamishi katika KPS na makao makuu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI), hakuna hatua iliyochukuliwa. Malalamiko makuu yalitoka kwa afisa kutoka Kituo cha Polisi cha Dandora ambaye alimshutumu Samir kwa kumbaka katika ofisi ya ripoti usiku sana.

IG baada ya kupokea faili ya IAU alitoa maagizo kwamba faili hiyo iwasilishwe kwa ODPP ili kukagua matokeo na kubaini njia ya kuendelea.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliafikiana na IAU na kuagiza afisa huyo ashtakiwe.