Rais Zelensky wa Ukraine afanya mazungumzo na Rais Ruto wa Kenya

Rais wa Ukraine alisema walijadili usalama wa chakula na mpango wa Nafaka kutoka Ukraine.

Muhtasari

•Bw Zelensky alisema walizungumza kuhusu kuundwa kwa hifadhi za nafaka barani Afrika, na kukubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Image: BBC

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amefanya mazungumzo na mwenzake wa Kenya William Ruto.

Katika mtandao wake wa twitter, rais wa Ukraine alisema walijadili usalama wa chakula na mpango wa Nafaka kutoka Ukraine - mpango wa kibinadamu wa kupeleka nafaka ya Ukraine kwa nchi zenye uhaba mkubwa wa chakula.

Bw Zelensky alisema pia walizungumza kuhusu kuundwa kwa hifadhi za nafaka barani Afrika, na kukubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Ukraine pia aliishukuru Kenya kwa msaada wake na "ushirikiano wa kujenga katika Umoja wa Mataifa" wakati wa vita nchini mwake vilivyoanza baada ya uvamizi wa Urusi Februari mwaka jana.

Ofisi ya rais wa Kenya haijatoa tamko lolote kuhusiana na mazungumzo hayo ya Alhamisi.

Kenya ilipinga uvamizi wa Urusi katika hotuba iliyowasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mara baada ya vita kuanza.

Mnamo Septemba, Bw Ruto alisema amejitolea kutekeleza jukumu kuu la ushirikiano katika ngazi ya kimataifa katika kutatua mgogoro wa Ukraine.