Wachumba wafariki baada ya gari lao kutumbukia kwenye bwawa

"Nilimsikia mwanamke akipiga kelele, alikuwa ndani ya bwawa akijaribu kuogelea, akijaribu kujiokoa

Muhtasari
  • Katika kingo za bwawa, chupa za pombe zinaonekana zikiwa zimetawanyika kila mahali jambo linaloonyesha wazi kuwa watu mara nyingi husherehekea eneo hilo
Image: KWA HISANI

Wachumba walifariki Jumanne usiku baada ya gari walilokuwamo kutumbukia kwenye bwawa la Titanic eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu.

Kulingana na wenyeji, wawili hao walikuwa ndani ya gari hilo lililokuwa limeegeshwa mita chache kutoka kwenye bwawa hilo na mwendo wa saa 7.30 usiku, walisikia watu wakipiga kelele za kuomba msaada.

"Nilimsikia mwanamke akipiga kelele, alikuwa ndani ya bwawa akijaribu kuogelea, akijaribu kujiokoa lakini kwa bahati mbaya hakukuwa na wapigambizi karibu. Baada ya gari kutumbukia ndani ya bwawa mwanamke huyo alifanikiwa kutoka nje ya gari kupitia madirisha,"mkazi wa eneo hilo alisema.

Katika kingo za bwawa, chupa za pombe zinaonekana zikiwa zimetawanyika kila mahali jambo linaloonyesha wazi kuwa watu mara nyingi husherehekea eneo hilo.

"Wanaegesha na kutulia hapa kila siku lakini wikendi huwezi hata kupata eneo la kuegesha magari hapa, wanamiminika hapa, wakinywa na kujiburudisha hapa. Hiki si kisa cha kwanza."