Fahamu jinsi ya kuangalia matokeo ya mtihani wa KCSE 2022

Machogu alitoa matokeo ya watahiniwa 881,416 waliofanya KCSE.

Muhtasari

•Watahiniwa sasa wanaweza kujua alama walizopata kupitia tovuti ya Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC).

•Watahiniwa pia naweza kupata matokeo kupitia njia ya SMS, kwenye ofisi za elimu za kaunti na shule zao.

wakati wa kuachiwa kwa matokeo ya KCSE katika Jumba la Mitihani huko Kilimani, Nairobi mnamo Januari 20, 2023.
Waziri wa elimu Ezekiel Machogu wakati wa kuachiwa kwa matokeo ya KCSE katika Jumba la Mitihani huko Kilimani, Nairobi mnamo Januari 20, 2023.
Image: ANDREW KASUKU

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alitoa matokeo ya KCSE 2022 siku ya Ijumaa, Januari 20.

Kufuatia kuachiliwa kwa matokeo hayo, watahiniwa sasa wanaweza kujua alama walizopata kupitia tovuti ya Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC).

“Watahiniwa watachukua matokeo yao kutoka katika vituo husika vya mitihani,” Machogu alisema.

Wale wanaotumia tovuti hiyo wanashauriwa kuelekea kwenye sehemu ya KCSE na kuchagua mwaka waliofanya mtihani wao wa kitaifa na kuandika nambari zao za usajili.

Watahiniwa pia naweza kupata matokeo kupitia njia ya SMS, kwenye ofisi za elimu za kaunti na shule zao.

Kwa wale wanaotumia mfumo wa SMS,Waziri alisema wazazi, walezi na wanafunzi wanapaswa kutuma nambari zao za usajili, zikifuatiwa na jina KCSE (kwa herufi kubwa) kwa 20076 ili kupata matokeo.

Mfumo wa SMS unapatikana kwa mitandao yote ya simu na itatozwa Sh25 kila moja.

CS Machogu alitoa matokeo ya watahiniwa 881,416 waliofanya mitihani ya Kitaifa.

Usahihishaji wa KCSE ulianza tarehe 28 Desemba 2022 hadi Januari 18, 2023.

Baraza la mitihani lilihusisha huduma za watahini 30,000 katika vituo 35.