NSAC ilitaka Raila Odinga atangazwe mshindi-Guliye

Guliye alitoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo inayoongozwa na Jaji Aggrey Muchelule Jumatatu

Muhtasari
  • Kulingana na hati ya kiapo ya Guliye, mwenyekiti wa wakati huo Wafula Chebukati alikubali wito huo lakini alilazimika kuahirisha mkutano huo hadi saa 2:00 adhuhuri
Kamishna wa IEBC Abdi Guliye
Image: WILFRED NYANGARESI

Aliyekuwa kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Abdi Guliye sasa anadai kuwa saa chache kabla ya kutangaza matokeo ya urais wa Agosti 2022, waliambiwa wamtangaze kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga kuwa mshindi  wa uchaguzi huo.

Guliye alitoa ushahidi mbele ya kamati ya uchunguzi wa uchaguzi inayoongozwa na Jaji Aggrey Muchelule Jumatatu akisema kwamba mnamo Agosti 15, 2022, saa chache kabla ya kutangaza matokeo ya mwisho ya urais, timu ya wageni wanne walidai kuhudhuria kikao pamoja na makamishna wote mwendo wa saa nne asubuhi.

Kulingana na hati ya kiapo ya Guliye, mwenyekiti wa wakati huo Wafula Chebukati alikubali wito huo lakini alilazimika kuahirisha mkutano huo hadi saa nane alasiri kwa sababu alikuwa anakamilisha baadhi ya michakato ya uhakiki wa kura.

“Walitaka kumuona mwenyekiti na akasema tutaonana lakini alikuwa anamalizia kwanza baadhi ya taratibu za uhakiki na tutawaona saa mbili kamili,” alibainisha.

Guliye aliendelea kusema kuwa katika muda uliopangwa upya, Chebukati aliwaita wote, wakiwemo wageni hao wanne, kwenye chumba cha mikutano cha Mkurugenzi Mtendaji wa Bomas.

"Tulipokaribia kumaliza, mwenyekiti aliitisha mkutano saa 2 jioni na huu ulikuwa mkutano wa makamishna na matarajio yetu yalikuwa kwamba matokeo ya mwisho yangechapishwa,"alisema.

Guliye alisema kuwa timu hiyo ya watu wanne ilitambulishwa, na wakasema kwamba walikuwa hapo kwa niaba ya Kamati ya Ushauri ya Usalama wa Kitaifa (NSAC).