Tuju na Wako walitaka IEBC ibadilishe uchaguzi - Chebukati

Chebukati alisema kuwa Juju alikuwa amewaahidi makamishna zawadi nono ikiwa wangekubali kutekeleza ombi lao.

Muhtasari

• Chebukati pia alidai kushawishiwa na baadhi ya wanachama wa kamati ya usalama wa kitaifa kutomtangaza Ruto kama mshindi wa uchaguzi.

Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika jopo la kumchunguza kamishna Irene Masit.
Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika jopo la kumchunguza kamishna Irene Masit.
Image: Star

Aliyekuwa seneta wa Busia Amos Wako na aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju walitaka tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kubalisha matokeo ya uchaguzi wa urais 2022.

Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitoa madai hayo siku ya Jumanne wakati wa kikao cha jopo maalum lililoundwa na rais William Ruto kumchunguza kamishma wa IEBC Irene Masit.

Katika madai ya kina Chebukati alidai kuwa Tuju na Wako walitaka tume hiyo kuhakikisha kuwa Ruto hatangazwi mshindi wa uchaguzi na badala yake kumtangaza mgombea wa Azimio Raila Odinga kama mshindi au wapunguze kura za Ruto ili walazimishe duru ya pili ya uchaguzi.

Chebukati alisema kuwa Tuju alikuwa amewaahidi makamishna hao zawadi nono ikiwa wangekubali kutekeleza ombi lao.

“Fikiria kuhusu ombi hili na utapewa zawadi nono”, Chebukati alisema.

Chebukati hata hivyo alisema kwamba alimweleza Tuju kuwa analipwa vyema kwa kazi yake na hataki zawadi yoyote kubadilisha matokeo ya uchaguzi.

Kulingana na chebukati Kamishna Masit aliomba makamishna wengine kukubali ombi la Tuju na Wako.

Mwenyekiti huyo wa IEBC ambaye kwa sasa amestaafu, hata hivyo aliambia jopo hilo kwamba yeye na baadhi ya makamishna walikataa kata kata ombi la Tuju na Wako.

Kulingana naye kamishna Massit alikuwa miongoni mwa makamisna waliotaka kuvuruga matokeo ya uchaguzi na kuwanyima wakenya haki kumchagua rais wanayemtaka.

Masit ndiye kamishna wa pekee kati ya wanne waliokuwa wamesimamishwa kazi kwa muda ili wachunguzwe kwa madai ya kukiuka kaununi za kusimamia uchaguzi. Watatu wakiwemo aliyekuwa naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi waliamua kujiuzulu badala ya kufika mbele ya jopo.

Katika kikao cha Jumanne Chebukati pia alidai kushawishiwa na baadhi ya wanachama wa kamati ya usalama wa kitaifa kutomtangaza Ruto kama mshindi wa uchaguzi. Alidai kuwa wanachama hao walikuwa wamedai kwamba kumtangaza Ruto mshindi kungezua rabsha nchini.  Kamati hiyo ilikuwa imemuambia kwamba ghasia zilikuwa tayari zimezuka katika baadhi ya maeno nchini.

Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika jopo la kumchunguza kamishna Irene Masit.
Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika jopo la kumchunguza kamishna Irene Masit.
Image: Star