Wafanyakazi wa chuo kikuu cha Machakos wagoma kulalamikia kucheleweshwa kupandishwa vyeo

Katibu Mkuu wa UASU wa Machakos Martin Kasina alikariri hisia hizo akisema masuala hayo yanavuka mipaka

Muhtasari
  • Katibu Mkuu wa UASU wa Machakos Martin Kasina alikariri hisia hizo akisema masuala hayo yanavuka mipaka na ni dhuluma tu kwa wanachama wao
Image: GEORGE OWITI

Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Machakos wameweka chini zana zao baada ya madai yao kudaiwa kutotatuliwa na wasimamizi wa taasisi hiyo, muhimu miongoni mwao kucheleweshwa na kunyimwa vyeo.

Wafanyakazi hao, kutoka Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu vya Kenya (KUSU) na Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (UASU), wanamshutumu Naibu Chansela wa chuo hicho Lucy Ndung'u kwa kukosa kutoa suluhu la amani kwa masaibu yao.

Wakihutubia wanahabari baada ya saa kadhaa za maandamano  katika majengo ya chuo hicho Jumanne, wafanyikazi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa KUSU wa Machakos Silvanus Mukai walisema usimamizi wa chuo hicho umeshindwa kuwapa vyeo wanachama wao kwa miaka 10 iliyopita.

Pia walitaka wanachama wa muungano ambao wako katika nafasi ya kaimu waidhinishwe na chuo kitekeleze Makubaliano ya Pamoja ya Majadiliano (CBA) 2016-2021.

Katika barua waliyoiandikia chuo hicho, walidai kuwa kumekuwa na watumishi wanaofanya kazi kwa mkataba kwa zaidi ya miaka mitano bila ya uthibitisho wa masharti ya kudumu na ya pensheni, jambo ambalo wanasema ni kinyume cha taratibu za kazi na Sheria ya Ajira ya mwaka 2007.

Mheshimiwa Mukai vile vile alibainisha kuwa baadhi ya watumishi wamekaa kwenye nafasi za kaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kuteuliwa katika nafasi hizo, jambo ambalo pia linakiuka sheria za kazi.

Katibu Mkuu wa UASU wa Machakos Martin Kasina alikariri hisia hizo akisema masuala hayo yanavuka mipaka na ni dhuluma tu kwa wanachama wao.

Maafisa wa muungano huo waliapa kuendelea na hatua yao ya kiviwanda hadi malalamishi yao yatashughulikiwa.