Mfanyikazi aliyeshambuliwa Albania kurejeshwa Kenya leo, Jumatano kwa matibabu maalum

Joyce alishambuliwa vibaya na watu wasiojulikana akiwa kazini mwake jijini Tirana, Albania.

Muhtasari

•Bi Joyce Aoko alishambuliwa vibaya na watu wasiojulikana akiwa kazini mwake jijini Tirana, Albania mnamo Agosti 2022 na kuugua majeraha mwilini ambayo yalihitaji matibabu maalum.

•Joyce aliwekwa kwenye ndege kutoka Albania siku ya Jumatano, Januari 25, na anatarajiwa kuwasili katika uwanja wa ndege wa Wilson, Kenya baadaye mwendo wa saa mbili jioni.

Ndege ya Kenya Airways
Image: MAKTABA

Serikali ya Kenya imeanzisha mchakato wa kumuhamisha mwanamke Mkenya ambaye amekuwa akiugua nchini Albania.

Bi Joyce Achieng' Aoko alishambuliwa vibaya na watu wasiojulikana akiwa kazini mwake jijini Tirana, Albania mnamo Agosti 2022 na kuugua majeraha mwilini ambayo yalihitaji matibabu maalum.

Idara ya serikali ya masuala ya Diaspora, katika taarifa ya siku ya Jumatano, imefichua kuwa Joyce alipelekwa hospitalini akiwa hali mahututi na kulazwa baada ya shambulio hilo lakini ikabainika alihitaji matibabu maalum ya mishipa ambayo hayakupatikana nchini Albania.

“Huku tukiendelea kuisihi serikali ya Jamhuri ya Albania uchunguzi wa haraka na kina ili kuwakamata wahalifu, tuliona inafaa kwa manufaa ya Bi Aoko, kumleta nyumbani ili kukamilisha safari yake ya mmalizi akiwa na mpendwa wake wale,” Idara hiyo ilisema.

Kufuatia hayo, Joyce aliwekwa kwenye ndege kutoka Albania siku ya Jumatano, Januari 25, na anatarajiwa kuwasili katika uwanja wa ndege wa Wilson, Kenya baadaye mwendo wa saa mbili jioni.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Diaspora, Bi Roseline K Njogu atakuwa katika uwanja wa ndege kumpokea Joyce kisha atapelekwa katika Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) kwa matibabu zaidi.

Wanafamilia wa mwathiriwa pia watapokea huduma ya ushauri nasaha bila malipo baada ya kuwasili.