Profesa George Magoha Kuzikwa Februari 11

Magoha 71, aliaga dunia Januari 24 katika hospitali ya Nairobi.

Muhtasari

•Julius Jwan alisema Magoha atazikwa katika eneo la Umiru‚ kaunti ndogo  ya Nyamininia.

•Viongozi mbali mbali wametembelea familia kuwapa rambirambi zao.

George Magoha
George Magoha
Image: Maktaba

Familia ya aliyekuwa waziri wa masomo Prof George Magoha imetangaza kuwa atazikwa Februari 11‚2023.

Kulingana na aliyekuwa  katibu wa kudumu wa elimu ya msingi‚Julius Jwan,  Magoha atazikwa katika eneo la Umiru‚ kaunti ndogo  ya Nyamininia.

Magoha aliaga dunia Januari 24 katika hospitali ya Nairobi akiwa na umri 71.

Tangu kutangazwa kwa kifo chake viongozi mbalimbali wameitembelea familia yake kuipa rambirambi zao na kuomboleza nao.

Msafara wa kumpa Magoha heshima za mwisho utafanyika Nairobi kabla ya mazishi Februari 11‚2023. 

Jwan anayeiongoza kamati ya mazishi ya Magoha alitangaza kuwa msafara huo utafanyika Februari 8.

''Msafara huo utapitia Chuo cha Sayansi ya Afya cha KNH ‚ofisi za KMPDU‚ KNEC ‚Shule ya Msingi ya ST Georges‚ Shule ya Upili ya Wasichana ya State House‚Chuo kikuu cha Nairobi‚na kumalizia katika Starehe Centre‚'' alisema Jwan.

Jwan aliedelea kusema kuwa Magoha alipenda kutangamana na wanafunzi na watoto.'

"Hii inaeleza kwa nini tunaangazia shule ambazo aliweza kuwa na athari kubwa kwa wanafunzi"

Misa ya wafu itaandaliwa Februari 9 katika kanisa la Consolata Shrine‚Westlands kuanzia saa tatu asubuhi.

Kwa kuongezea Jwan alisema kuwa mwili  wa Magoha utawasili Shule ya Msingi ya Yala Township Februari 10 kabla ya misa takatifu itakayofanyika nyumbani kwa marehemu‚ Umiru‚ Nyamininia.

Misa ya mazishi itafanyika  katika Chuo Kikuu cha Odera Kang'o  katika eneo la Yala Februari 11‚kuanzia saa nne subuhi.