Magari mawili yateketea kufuatia ajali ya barabarani Machakos

Polisi na raia walikuwa kwenye eneo la tukio wakisaidia kuzima moto huo.

Muhtasari

•Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Machakos, Moss Ndhiwa alisema magari hayo ni trela ya futi 40 na gari la saloon.

Tukio la ajali ambapo magari mawili yaliteketea kwa moto kufuatia ajali ya barabarani katika mji wa Machakos mnamo Alhamisi, Februari 16, 2023.
Tukio la ajali ambapo magari mawili yaliteketea kwa moto kufuatia ajali ya barabarani katika mji wa Machakos mnamo Alhamisi, Februari 16, 2023.
Image: GEORGE OWITI

Magari mawili yaliteketea Alhamisi usiku baada ya kushika moto kufuatia ajali iliyotokea katika mji wa Machakos.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Machakos, Moss Ndhiwa alisema magari hayo ni trela ya futi 40 na gari la saloon.

Ndhiwa alisema tukio hilo lilitokea kati ya vituo vya mafuta vya Shell na Rubis kwenye barabara ya Kyumbi-Machakos, mita chache kutoka Kituo cha Susu.

"Magari hayo mawili yaliungua kufuatia ajali ya barabarani. Tunajaribu kuuzima," Ndhiwa alisema kwenye simu Alhamisi usiku.

Alisema tukio hilo lilitokea dakika chache baada ya saa mbili jioni.

"Hatuwezi kutoa maelezo sasa, tuzime moto kwanza. Nitatoa maelezo baadaye," bosi huyo wa polisi aliongeza.

Polisi na raia walikuwa kwenye eneo la tukio wakisaidia kuzima moto huo.