Watu wanaoshukiwa kuwa wezi walivamia nyumba za maafisa wa polisi katika eneo la Busia na kuiba bunduki, silinda ya gesi na redio mbili.
Kisa hicho kilitokea katika eneo la Milimani Estate karibu na mpaka wa Kenya na Uganda.
Inashukiwa mmoja wa waathiriwa alipuliziwa dawa ya kupoteza fahamu kabla ya kuibiwa.
Afisa huyo wa Polisi alikuwa ameenda nyumbani kwake mwendo wa saatatu unusu usiku wa Jumamosi. Aliamka Jumapili asubuhi na kukuta chumba chake kikiwa kimepanguliwa.
"Aliamka akiwa na maumivu ya kichwa na alikuwa akihisi kizunguzungu ndipo akagundua koti lake lililowekwa karibu na kitanda chake likiwa chini na nguo zimetawanyika kila mahali," polisi walisema.
Baadaye aligundua kuwa bunduki yake, bastola ya Czeska, pamoja na risasi 15 hazikuwepo kwenye koti lake.
Kisha alitoa taarifa kwa vitengo vya polisi katika kaunti hiyo ambao walifika eneo la tukio na kubaini kuwa wezi hao walivamia nyumba kupitia mlango wa nyuma baada ya kunyunyizia chumba hicho dawa ya kusababisha kupoteza fahamu.
Polisi walisema watu hao wasiojulikana pia walivamia nyumba nyingine ya afisa mwingine ambaye wakati huo hakuwa ndani ya nyumba hiyo.
Silinda ya gesi ya kilo sita na redio ziliibiwa kutoka kwa nyumba kubwa na redio nyingine kutoka kwa makazi ya wafanyikazi.
Msako ulifanyika eneo la tukio bila mafanikio. Mbwa wa polisi aliletwa kwenye eneo la tukio na kuchukua harufu ambayo ilimpeleka kwenye barabara kuu inayoelekea Uganda lakini ikatoweka kabla ya kufika kwenye mpaka.
Polisi waliotembelea eneo la tukio walisema hakuna mafanikio yaliyopatikana lakini juhudi za kuwapata washukiwa hao zinaendelea.