Aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori akutana na Atwoli, Gumo na Wako

Awori ambaye ana umri wa miaka 94 alionekana mkakamavu na mwenye furaha.

Muhtasari

• Leo asubuhi pamoja na Mwanasheria Mkuu Mstaafu Seneta Amos Wako na Mhe. Fred Gumo, tulimtembelea aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya Mhe. Arthur Moody Awori akiwa nyumbani kwake Lavington - Atwoli.

Aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori (wa pili kushoto) akiwa na viongozi kutoka magharibi waliomtembelea nyumbani kwake mtaani Lavington Nairobi, 8/3/2023.
Aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori (wa pili kushoto) akiwa na viongozi kutoka magharibi waliomtembelea nyumbani kwake mtaani Lavington Nairobi, 8/3/2023.
Image: HISANI

Aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori siku ya Jumatano alikuwa mwenyeji wa baadhi ya viongozi kutoka eneo la magharibi.

Katibu mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini Francis Atwoli, mwanasheria mkuu mstaafu na ambaye pia alikuwa seneta wa Busia Amos pamoja na aliyekuwa mbunge wa Westlands Fred Gumo walimtembelea Awori nyumbani kwake mtaani Lavington Nairobi, mapema siku ya Jumatano.

“Leo asubuhi pamoja na Mwanasheria Mkuu Mstaafu Seneta Amos Wako na Mhe. Fred Gumo, tulimtembelea aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya Mhe. Arthur Moody Awori akiwa nyumbani kwake Lavington.,” Atwoli aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Image: HISANI

Awori ambaye ana umri wa miaka 94 alionekana mkakamavu na mwenye furaha huku akizungumza na viongozi wenzake kutoka magharibi. Atwoli alitundika kwenye mtandao wa Twitter picha za viongozi hao wakipiga gumzo na Uncle Moody kama anavyojulikana na wengi.

“Ilikuwa vizuri sana kujadiliana na Mhe. Moody na kukumbushana kuhusu masuala mengi ya manufaa ya kila mmoja wetu,” Atwoli aliongeza.

Awori alikuwa mbunge wa Funyula kwa jumla ya miaka 24, baada ya kumshinda kura aliyekuwa mbunge Julia Ojiambo katika uchaguzi wa mwaka 1983 hadi mwaka 2007.

Alikuwa na safari ya kufana katika siasa ambapo alihudumu kama waziri msaidizi kwa miaka mingi katika serikali ya hayati rais Daniel Moi, kabla ya kuteuliwa waziri na makamu wa rais katika serikali ya hayati rais Mwai Kibaki.

Safari ya viongozi hawa watatu inajiri baada ya uvumi kuibuka kuhusu hali ya mzee Awori uvumi ambao ulipuuziliwa mbali na familia yake.