Kenya yaanzisha msako dhidi ya LGBTQ shuleni

Kamati tayari imeundwa kushughulikia masuala ya LGBTQ shuleni.

Muhtasari

•Wizara imeanzisha msako mkali dhidi ya kile ilichotaja kuwa kupenyezwa kwa ajenda ya LGBTQ shuleni.

•Kuna hofu kwamba programu inaweza kuwa na Habari za watu wa LGBTQ na uhusiano wa jinsia moja kufundishwa shuleni.

Image: BBC

Wizara ya elimu nchini Kenya imeanzisha msako mkali dhidi ya kile ilichotaja kuwa kupenyezwa kwa ajenda ya LGBTQ shuleni.

Hatua hiyo itapekelekea serikali kuanzisha kitengo cha viongozi wa dini shuleni, waziri Ezekiel Machogu aliwaambia maseneta siku ya Alhamisi.

Kuna hofu kwamba programu inaweza kuwa na Habari za watu wa LGBTQ na uhusiano wa jinsia moja kufundishwa shuleni.

Mapenzi ya jinsia moja bado ni kinyume cha sheria lakini mitazamo dhidi ya LGBTQ imekuwa ikiongezeka kufuatia uamuzi wa mwezi uliopita wa Mahakama ya Juu kwamba jamii hiyo ina haki ya kusajili chama chao.

Kamati tayari imeundwa kushughulikia masuala ya LGBTQ shuleni, waziri alisema, na kupendekeza jukumu lake linaweza kujumuisha kupitia upya mtaala shuleni.

Kamati hiyo itaongozwa na askofu mkuu kutoka kanisa la kianglikana nchini Kenya.

“Haya ni masuala ambayo hatuwezi kuruhusu yaingie katika shule zetu,” Bw Machogu alisema.

Waziri huyo alikuwa akimjibu seneta ambaye alikuwa na wasiwasi juu ya madai ya kuenea kwa ajenda ya LGBTQ katika shule za msingi.