Ofisi ya mke wangu haifadhiliwi na Wakenya- Mudavadi

Mudavadi alisema haoni afisi hiyo ikigharimu matumizi yoyote ya fedha za umma.

Muhtasari

•Raila alisema kuundwa kwa afisi hizo ikiwa ni pamoja na ile ya Mke wa Waziri Mkuu iliyotengewa mke wa Mudavadi, Tessie kunawalemea walipa ushuru.

•Mudavadi alisema kinyume na mawazo ya Raila, hakuna hata senti moja iliyotumika katika uendeshaji wa shughuli za afisi ya mkewe.

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi akihutubia wanahabari mjini Nairobi mnamo 19/01/2023
Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi akihutubia wanahabari mjini Nairobi mnamo 19/01/2023
Image: ANDREW KASUKU

Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi amejibu madai ya Raila Odinga kwamba Rais William Ruto ameongeza bili ya mishahara ambayo tayari ni kubwa kwa kuunda ofisi za umma zisizo za lazima.

Raila alisema kuundwa kwa afisi hizo ikiwa ni pamoja na ile ya Mke wa Waziri Mkuu iliyotengewa mke wa Mudavadi, Tessie kunawalemea walipa ushuru.

“Kuundwa kwa afisi zisizo za lazima na zisizo za kikatiba katika utumishi wa umma zikiwemo za wenzi wao, mabinti na wana wao kwa gharama ya raia ambao tayari wameelemewa na hazina tupu ni mbinu ya kikatili ya Ruto ya kuwatuza wandani wake,” Raila alisema.

"Kwa sababu hii, Ruto lazima aondoke," Raila alisema alipozindua rasmi maandamano ya Azimio siku ya Alhamisi katika makao makuu ya Jaramogi Oginga Odinga Foundation jijini Nairobi.

Lakini Mudavadi alisema kinyume na mawazo ya Raila, hakuna hata senti moja iliyotumika katika uendeshaji wa shughuli za afisi ya mkewe.

"Kutoka kwa kiwango cha kibinafsi, ikiwa nitazungumza haswa kama Musalia Mudavadi, nataka kusema wazi kwamba hakuna matumizi ya pesa za umma ambayo yametokea katika mazungumzo kuhusu Tessie Musalia," alisema.

Waziri Mkuu alikuwa akizungumza wakati wa Tamasha la People Dialogue katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Kenya jijini Nairobi.

Mudavadi alisema haoni afisi hiyo ikigharimu matumizi yoyote ya fedha za umma siku za usoni kwa vile shughuli anazofanya mkewe si za Serikali.

"Ni kazi za kijamii, za hisani tunazofanya. Na ili kuepusha shaka, Bi Musalia Mudavadi amekuwa katika mchakato huu nikiwa serikalini na hata kama sikuwa serikalini," alisema.

Mudavadi alisema hawataacha kuunga mkono raia wanaohitaji msaada katika sehemu yoyote ya nchi kupitia mashirika ya hisani lakini akasisitiza kuwa hilo halitatekelezwa kupitia matumizi ya pesa za umma.

Wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo Februari 24, Mudavadi alisema Ofisi ya Mke wa Katibu Mkuu itakamilisha kazi inayofanywa na mabibi wa kwanza na wa pili nchini.