IPOA yaanzisha uchunguzi wa mauaji ya wanaume 2 Murang'a

Katika taarifa kutoka kwa mwenyekiti Anne Makori siku ya Jumatatu, IPOA ilisema timu tayari imetumwa katika eneo hilo

Muhtasari
  • Katika taarifa kutoka kwa mwenyekiti Anne Makori siku ya Jumatatu, IPOA ilisema timu tayari imetumwa katika eneo hilo
Anne Makori mwneyekiti wa IPOA

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya wanaume wawili waliouawa kwa kupigwa risasi Jumapili Murang'a.

Katika taarifa kutoka kwa mwenyekiti Anne Makori siku ya Jumatatu, IPOA ilisema timu tayari imetumwa katika eneo hilo na tangu wakati huo imebaini kuwa maafisa wa polisi walikuwa sehemu ya tukio hilo.

Makori aliongeza kuwa hatua zinazofaa zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Haya yanajiri huku kukiwa na maswali mengi kutoka kwa umma baada ya kifo cha wawili hao kuripotiwa kwa njia isiyo ya kawaida na Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

DCI, katika kisa hicho, iliripoti kuwa washukiwa hao walipigwa risasi baada ya "makabiliano makali ya risasi na maafisa wa polisi" katika eneo la Kigumo, kaunti ya Murang’a Jumapili asubuhi.

Ripoti hiyo ilizua hisia tofauti mitandaoni baada ya uvumi kuwa maafisa wa polisi walikuwa wamewakamata wawili hao hapo awali.