logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Inspekta Jenerali Koome atishia kuwakamata viongozi wa Azimio juu ya maandamano

Polisi wameonya dhidi ya mikusanyiko yoyote ya watu wengi ama maandamano wakisema kuwa ni kinyume cha sheria.

image
na

Habari26 March 2023 - 10:00

Muhtasari


•Koome ametishia kuwakamata viongozi wakuu, ikiwa ni pamoja na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ikiwa watajaribu kufanya maandamano siku ya Jumatatu na Alhamisi.

•Alisema yeyote atakayekutwa na silaha za kushambulia na kusababisha fujo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome

Inspekta Jenerali wa polisi Japheth Koome ametishia kuwakamata viongozi wakuu, ikiwa ni pamoja na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ikiwa watajaribu kufanya maandamano siku ya Jumatatu na Alhamisi.

Polisi wameonya dhidi ya mikusanyiko yoyote ya watu wengi ama maandamano wakisema kuwa ni kinyume cha sheria.

Siku ya Jumapili, IG alisema kwamba polisi watawatendea kila mtu kwa usawa wakati wa kuwakamata waandamanaji mitaani.

Koome, alipokuwa akihutubia wanahabari alisema hata makamanda wake hawatajali hadhi ya mtu yeyote katika jamii wanapokabiliana na waandamanaji.

"Hata iwe ni nani, nitakushughulikia," Koome alisema.

Matamshi ya IG yalionekana kulenga viongozi wakuu wa Azimio akiwemo Raila, mkuu wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua.

IG alisema kuwa hakutakuwa na utaratibu maalum kwa mtu yeyote wakati wa kuwakamata waandamanaji ikiwa ni pamoja na wale ambao watakuwa wamebebwa kwenye magari makubwa kama Prado.

"Uko kiwango gani katika jamii, upo katika hadhi gani. Nina land cruiser za kutosha kukuweka upande wa nyuma. Kesho siweki mtu kwenye Prado. Nitakayemkamata kesho nitakuweka kwenye Landcruiser, utakwenda jela na kukaa huko milele," Koome alisema.

Alisema yeyote atakayekutwa na silaha za kushambulia na kusababisha fujo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Koome alisema silaha za mashambulizi ni pamoja na mawe, rungu, panga pamoja na zana zingine.

"Ikiwa una nia ya kusababisha fujo, na umejihami kwa kile tunachoita silaha za kudhuru, mawe, rungu na mapanga utakabiliwa nawe," Koome alisema.

Koome alikuwa akizungumza kuhusu maandamano yaliyopangwa Jumatatu.

Upinzani umewataka wafuasi wake kujitokeza barabarani siku ya Jumatatu na Alhamisi kuandamana dhidi ya uongozi wa Rais William Ruto.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved