logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mmoja afariki, 23 wajeruhiwa huku magari yakiteketea Mombasa Road

Mtu mmoja amefariki huku wengine 23 wakipata majeraha mabaya baada ya magari mawili kuwaka moto Mombasa Road.

image
na Samuel Maina

Habari21 April 2023 - 07:47

Muhtasari


  • •Napeiyan alisema mtu aliyefariki ni dereva wa Toyota Hilux huku majeruhi wakiwa ni abiria waliokuwa ndani ya basi.
  • •Dereva wa Pickup alichomwa moto kiasi cha kutotambulika.
ambayo yaliteketea kwa moto kando ya barabara ya Mombasa katika eneo la Maanzoni Lodge huko Athi River, Kaunti ya Machakos mnamo Ijumaa, Aprili 21, 2023.

Mtu mmoja amefariki huku wengine 23 wakipata majeraha mabaya baada ya magari mawili kuwaka moto katika barabara ya Mombasa.

Mkuu wa polisi katika Kaunti ya Machakos Joseph Ole Napeiyan alisema basi la abiria na gari la Toyota Hilux ziligongana uso kwa uso kabla ya kuteketea kwa moto Ijumaa usiku.

Ajali hiyo, kulingana na Napeiyan, ilitokea kwenye barabara kuu ya Nairobi - Mombasa karibu na kituo cha mafuta cha Shell, mita chache kutoka Maanzoni Lodge, eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Ijumaa. 

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Kyumbi eneo la Makutano Junction, Kaunti ya Machakos.

Napeiyan alisema mtu aliyefariki ni dereva wa Toyota Hilux huku majeruhi wakiwa ni abiria waliokuwa ndani ya basi.

Marehemu hakutambuliwa mara moja.

"Toyota Hilux iliyokuwa ikielekea Nairobi iligongana uso kwa uso na gari lililokuwa likija," Napeiyan alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, dereva wa pickup alinaswa ndani ya gari hilo ambalo liliwaka moto. Alichomwa moto kiasi cha kutotambulika.

“Dereva wa basi na abiria walijeruhiwa baada ya magari hayo kuwaka moto. Moto huo ulizimwa na kikosi cha wazima moto kutoka serikali ya Kaunti ya Machakos,” Napeiyan alisema.

Mkuu huyo wa polisi alisema majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali ya Machakos Level 5 na wanaendelea na matibabu huku marehemu akipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti akisubiri kufanyiwa uchunguzi na kutambuliwa.

Mabaki ya magari yalivutwa hadi kituo cha polisi cha Kyumbi kwa ukaguzi.

Napeiyan alisema maafisa kutoka idara ya trafiki kituo cha polisi cha Kyumbi wameanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo.

Aliwaonya madereva dhidi ya kukiuka sheria za trafiki ili kupunguza visa vya ajali.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved