CS Kindiki amtaka mchungaji Mackenzie kushtakiwa kwa mauaji ya halaiki katika mahakama ya ICC

Kindiki vile vile alitoa wito wa kuwepo kwa mbinu shirikishi kusaidia katika kuokoa maisha ya wale ambao huenda wameathiriwa

Muhtasari
  • Jumla ya miili 16 ya ziada ilikuwa imeopolewa na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia 89 huku watu watatu pia wakiokolewa.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KITHURE KINDIKI
Image: KWA HISANI

Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki amependekeza kuwa kasisi Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International Church huko Malindi ashtakiwe kwa ugaidi na mauaji ya halaiki kufuatia mafundisho yake yenye utata yaliyosababisha wafuasi wake kufunga hadi kifo.

Waziri huyo alizungumza alipozuru msitu wa Shakahola siku ya Jumanne kutathmini hali ilivyo huku shughuli ya kuwafukua miili ya wafuasi wa Mackenzie 'waliochanganyikiwa' ikiendelea hadi siku ya tano.

Inasemekana kwamba kundi la Mackenzie lilitii mafundisho yake kwa matumaini ya 'kukutana na Mungu.'

Kulingana na Kindiki, vitendo vya Mackenzie ni sawa na mauaji ya halaiki na pasta huyo anapaswa kuwasilishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kujibu kwa ukatili wake.

"Inawezekana kumshtaki kwa mauaji ya halaiki katika ICC. Pia tunafuatilia washirika wake wanaojulikana," alisema CS.

Kindiki vile vile alitoa wito wa kuwepo kwa mbinu shirikishi kusaidia katika kuokoa maisha ya wale ambao huenda wameathiriwa na mafundisho ya kidini yenye itikadi kali ya Mackenzie.

"Kuanzia leo tumeongeza uokoaji; tunaongeza wafanyikazi. Operesheni ya mashirika mengi ya utafutaji na uokoaji itahusisha mashirika yote na itaongozwa na usalama," alisema CS.

"Tutaimarisha sheria zinazoongoza mashirika ya kidini. Mhubiri yeyote, anayehubiri ujumbe wowote unaopingana na Katiba ya Kenya au kushiriki katika uhalifu lazima akomeshwe. Lazima kuwe na uwajibikaji."

Jumla ya miili 16 ya ziada ilikuwa imeopolewa na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia 89 huku watu watatu pia wakiokolewa.