MCK yalaani polisi kwa kuzuia vyombo vya habari kuripoti mkasa wa Shakahola

Katika taarifa, MCK ilisema hatua hiyo inanyima vyombo vya habari kupata taarifa kuhusu suala la maslahi ya umma.

Muhtasari
  • Siku ya Jumatano, vyombo vya habari vilizuiwa kwenda kwenye Msitu wa Shakahola na polisi.
  • Ardhi hiyo ya ekari 800 inamilikiwa na Mchungaji Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International Church.
MCK yalaani polisi kwa kuzuia vyombo vya habari kuripoti mkasa wa Shakahola
Image: MCK/TWITTER

Baraza la Habari nchini Kenya limewalaani polisi kwa kuwafungia nje wanahabari waliokuwa wakiripoti mkasa wa Shakahola.

Katika taarifa, MCK ilisema hatua hiyo inanyima vyombo vya habari kupata taarifa kuhusu suala la maslahi ya umma.

"Hii itafungua milango ya taarifa potofu, uvumi na mkanganyiko kwa nchi nzima. Inakiuka kanuni za uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari," ilisoma taarifa hiyo.

Siku ya Jumatano, vyombo vya habari vilizuiwa kwenda kwenye Msitu wa Shakahola na polisi.

Ardhi hiyo ya ekari 800 inamilikiwa na Mchungaji Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International Church.

Mackenzie anashukiwa kuwafundisha wafuasi wa kanisa lake kufunga hadi kufa kwa imani ya kupaa mbinguni kukutana na Yesu Kristo.

Mnamo Jumanne, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alitoa amri ya kutotoka nje kwa siku 30 kutoka jioni hadi alfajiri katika eneo la Chakama Ranch.

"Sehemu nzima ya ardhi ya ekari 800 ambayo ni sehemu ya ranchi ya Shakahola inatangazwa kuwa eneo lenye misukosuko na eneo la operesheni. Timu ya wakala mbalimbali ya usalama itaongeza misheni ya utafutaji na uokoaji ili kuokoa maisha ya watu wengi iwezekanavyo,” alisema.

Kindiki alisema serikali ilituma askari zaidi wa usalama kuvuka msitu mkubwa wa Shakahola kuokoa wafuasi waliosalia.

Matamshi yake yanakuja baada ya takriban miili 95 kuopolewa kutoka kwenye makaburi katika msitu huo.

Zaidi ya watu 360 hawajulikani waliko huku ufukuzi na uokoqaji ukiendelea eneo hilo.