Ziara ya mchungaji Ezekiel yasababisha msongmano Nairobi

Mamia walimiminika katika eneo la Miracle Maximum Center Jumatano asubuhi kukutana na Mchungaji Ezekiel Odero.

Muhtasari

• Wafuasi hao walisababisha msongamano mkubwa na kuathiri mtiririko wa kawaida wa magari kuingia na kutoka kwenye kituo cha magari cha Odeon Cinema.

• Mhubiri huyo anachunguzwa kuhusu madai ya kuwapa wafuasi wake mahubiri ya itikadi kali.

Wakazi wa Nairobi wakusanyika nje ya kituo cha Maximum Miracle Centre cha Pastor Muiru ili kumuona Mchungaji Ezekiel kwenye ziara yake. Picha: SCREENGRAB
Wakazi wa Nairobi wakusanyika nje ya kituo cha Maximum Miracle Centre cha Pastor Muiru ili kumuona Mchungaji Ezekiel kwenye ziara yake. Picha: SCREENGRAB

Wafuasi wa mhubiri Pius Muiru Jumatano asubuhi walimiminika katika eneo la Miracle Maximum Center kukutana na Mchungaji Ezekiel Odero.

Kanisa lilijaa pomoni na kuwalazimisha waumini wengine kufuata mahubiri nje ya kanisa na kando ya barabara za Nairobi.

"Kwanzia leo nimepona na nimeokoka," wafuasi walipiga kelele nje ya kanisa.

Walisema hivi kwa 'amri' ya Ezekieli ambaye aliwaagiza kurudia maneno baada yake.

Wafuasi hao walisababisha msongamano mkubwa na kuathiri mtiririko wa kawaida wa magari kuingia na kutoka kwenye kituo cha magari cha Odeon Cinema na barabara za karibu.

Ezekiel anazuru kanisa la Muiru kwa mara ya kwanza tangu awachiliwe kutoka korokoroni. Wafuasi wake na wa Muiru wote walikusanyika kanisani kusikiliza mahubiri yake.

Aliachiliwa kwa sharti la kuripoti kituo cha polisi mara moja kwa wiki au kama inavyotakiwa na polisi.

Ezekiel pia aliamriwa ajizuie kuzungumzia suala la Shakahola.

Mhubiri huyo anachunguzwa kuhusu madai ya kuwapa wafuasi wake mahubiri ya itikadi kali.

Kwa sasa yuko nje kwa bondi ya Shilingi milioni 3 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au dhamana ya pesa taslimu milioni Sh1.5.

Mchungaji Ezekiel amehusishwa na mhubiri mwenye utata kutoka Malindi Paul Mackenzie ambaye shamba lake la ekari 800 kumefukukuliwa zaidi ya maiti 200. Hata hivyo, amekana kosa lolote.

Kanisa la News Life Prayer Center and Church lilisajiliwa mnamo Septemba 11, 2012, chini ya nambari ya usajili 3877.