Mkuu wa jeshi la Sudan anaonekana kwenye video ya kipekee akiwa na bunduki

Hii ni video ya kwanza ya aina yake tangu mzozo unaoendelea wa kijeshi uanze tarehe 15 Aprili.

Muhtasari

• Mkuu wa jeshi na mpinzani wake kamanda wa RSF Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti, wamejaribu kuongeza ari ya vikosi vyao vinavyopigana.

Image: Jeshi la Sudan/Facebook

Jeshi la Sudan limechapisha video inayoonyesha kiongozi wake, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, akitembea kati ya wanajeshi waliokuwa wakishangilia katika eneo lisilojulikana katika mji mkuu, Khartoum.

Video hiyo ya nadra ya sekunde 23 iliyochapishwa siku ya Jumatano inaonyesha Jenerali Burhan akiwa na bunduki na bastola.Anaonekana akiwa amevalia mavazi ya kijeshi, akiwasalimia wanajeshi wanaomshangilia .

"Mpiganaji - Kamanda Mkuu wa Majeshi - kati ya askari wake uwanjani," kichwa cha habari cha video hiyo kilisema.

Hii ni video ya kwanza ya aina yake tangu mzozo unaoendelea wa kijeshi uanze tarehe 15 Aprili kati ya jeshi na na kikosi maalum cha (RSF).

Hata hivyo, katika siku za mwanzo za mapigano, Jenerali Burhan alionekana pamoja na viongozi wengine wa kijeshi wakiwaamuru askari kutoka ndani ya jengo lisilojulikana mjini Khartoum.

Mkuu wa jeshi na mpinzani wake kamanda wa RSF Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti, wamejaribu kuongeza ari ya vikosi vyao vinavyopigana.

Hemedti pia alijitokeza katika eneo lisilojulikana huko Khartoum.Hivi majuzi pia alikanusha katika ujumbe wa sauti kwamba aliuawa.

Mapigano hayo ambayo yanachangiwa na mzozo wa madaraka kati ya Jenerali Burhan na Hemedti yameingia mwezi wa pili ambapo zaidi ya watu 800 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Image: BBC