Maafisa wa upelelezi kaunti ya Nakuru wanamsaka aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga kuhusiana na kupatikana kwa bunduki mbili na zaidi ya misokoto 90 ya bangi katika nyumba inayohusishwa naye.
"Moja ya bunduki zilizopatikana ni bastola ya kujitengenezea nyumbani iliyokuwa na uwezo wa kufyatua huku nyingine ikiwa ni Tokarev ambayo nambari yake ya usajili ilikuwa imeharibiwa."
Mkuu wa DCI Mohamed Amin alisema katika taarifa yake Jumatatu jioni kwamba vitu hivyo vilipatikana kufuatia msako mkali wa wapelelezi katika kijiji cha Ngomongo, eneo la Dundori.
Alisema risasi tatu za 9mm tupu pia zilikutwa zikiwa zimefichwa kwenye moja ya vyumba ndani ya nyumba hiyo.
Amin alisema maafisa hao waliwakamata washukiwa wanane wenye umri wa kati ya miaka 37 na 54 wakati wa msako huo.
"Taarifa yoyote kuhusu aliko kiongozi huyo wa zamani wa Mungiki ambaye huenda amejificha inaweza kutolewa kupitia nambari ya simu ya #FichuakwaDCI 0800 722 203," Amin alisema.
Mnamo Mei 12, Njenga alidai kuwa nyumba zake tatu huko Nairobi, Nakuru na Laikipia zilivamiwa na polisi.
Alisema timu hizo, ambazo zilifika kwa wakati mmoja saa kumi asubuhi nyumbani kwake Lavington, Karen na Nyandarua, ziliwaambia wafanyakazi kuwa walikuwa wakimtafuta.
Baadhi ya wafanyikazi katika makazi yake ya Nyahururu waliambia vyombo vya habari kuwa takriban maafisa 20 walivamia nyumba hiyo na kutaka kupekua nyumba hiyo.