Sing'atuki ng'o, naibu gavana wa Siaya William Oduol asema

Oduol alisema hakuwa mwoga na hatakubali kushinikizwa na yeyote kujiuzulu.

Muhtasari

• Alisema ikiwa atajiuzulu, wakaazi wa Siaya hawatakuwa na mtu wa kuwasemea.

• Naibu gavana huyo pia alimfokea mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kwa kutaka ajiuzulu.

• Oduol alisisitiza kuwa suala la kujiuzulu sio chaguo, akiongeza kuwa ikiwa atajiuzulu, wakaazi wa Siaya hawatakuwa na mtu wa kuwasemea.

Naibu gavana wa Siaya William Oduol amekariri kuwa kamwe hatajiuzulu.

Akizungumza katika runinga ya Citizen, Oduol alisema hakuwa mwoga na hatakubali kushinikizwa na yeyote kujiuzulu.

"Siogopi. Nina wafuasi wengi nyuma yangu. Nina wafuasi nyuma yangu," alisema.

"Jaribuni kunizuia kuingia ofisini kwangu. Mtagundua nina wafuasi," alisema.

Naibu gavana huyo pia alimfokea mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kwa kutaka ajiuzulu.

Wandayi ambaye ni katibu wa ODM wa masuala ya kisiasa siku ya Jumatatu alitoa taarifa akimtaka Oduol ajiuzulu mara moja ili kutoa nafasi kwa mtu mwingine akisema uhusiano kati ya Gavana Orengo na naibu wake umesambaratika.

Alitaja uhusiano kati ya viongozi hao wawili kuwa mbaya akisema utoaji wa huduma bora bila kukatizwa kwa wakazi wa Siaya haukuwa na uhakika katika mazingira yaliyopo.

Lakini Oduol alimshutumu Wandayi ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa kwa kuwa na nia ya kuwa gavana wa Siaya baada ya Orengo.

“Ana nia ya kuwa gavana. Alitaka kuwania kiti hicho katika uchaguzi uliopita lakini akashawishiwa na kiongozi wetu Raila Odinga kuweka kando azma yake,” alisema.

Ili kumaliza mkwamo huo, naibu gavana huyo alipendekeza kuwa ODM inafaa kuitisha mkutano kati yake na Orengo ili kujadili masuala haya.

"Katika mkutano kama huu, nitaweka mezani masuala yote ambayo nimekuwa nikizungumza na kumruhusu gavana kuyapinga," alisema.

Oduol alisisitiza kuwa suala la kujiuzulu sio chaguo, akiongeza kuwa ikiwa atajiuzulu, wakaazi wa Siaya hawatakuwa na mtu wa kuwasemea.

"Wafisadi watakuwa na uwanja wa kuchezea nikijiuzulu. Hilo halitafanyika," alisema.

DG alidai kuwa walikubali kabla ya uchaguzi kuwa Orengo angenipa majukumu katika baraza la mawaziri la Kaunti. Alisema makubaliano hayo yalikuwa tu ya mdomo.

"Kwa sababu ya taaluma yangu, nilitaka kushauri juu ya maswala ya fedha," alisema.

Oduol alidai kwamba alichaguliwa kama mgombea mwenza wa Orengo kwa sababu ya umaarufu wake.

"Tulianza kufanya kazi na gavana kwa njia nzuri. Tofauti zetu zilianza nilipoanza kuibua waswali kuhusu ufisadi," alisema.

Alieleza kuwa tofauti zao ziliongezeka wakati maafisa "wafisadi" katika utawala uliopita walipohifadhiwa.

"Hawa ni watu ambao wanachunguzwa na EACC na DCI kuhusu kutoweka kwa Shilingi bilioni," alisema.

Oduol alisema haya wakati kiongozi wa ODM Raila Odinga akizuru kaunti ya Siaya na kupokelewa na gavana James Orengo katika makao makuu ya kaunti ya Siaya.

Raila atakuwa katika eneo bunge la Ugenya kutoa misaada mbalimbali kwa waathiriwa wa mafuriko katika eneo hilo.