logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Moses Kuria anahitaji usaidizi, seneta Sifuna asema

Seneta alisema Kuria hakupaswa kuruhusiwa kuingia katika Seneti kusafisha utovu wake.

image
na Davis Ojiambo

Habari21 June 2023 - 13:26

Muhtasari


  • • Gadhabu za Kuria zilitokana na ufichuzi wa NTV, kudai kuwa baadhi ya mawaziri walihusika katika sakata ya kuagiza mafuta ya kupikia.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna sasa anasema mashambulizi ya Waziri wa Biashara Moses Kuria dhidi ya vyombo vya habari amekuwa akiyatekeleza kwa awamu na hivyo basi, waziri anahitaji usaidizi.

Seneta huyo alisema mipayuko ya Kuria haiwezi kulaumiwa kwa pombe kwa sababu dhana hiyo itakuwa potovu.

Sifuna alizungumza baada ya upande wa Azimio katika Seneti kuondoka mara tu Kuria alipowasili kujibu maswali yanayohusu wizara yake.

Seneta huyo alisema Kuria hakupaswa kuruhusiwa kuingia katika Seneti kusafisha utovu wake wa nidhamu.

"Kwa upande wa Moses Kuria, kulaumu pombe ni dhana potovu. Tatizo lake ni la kimfumo zaidi na anahitaji kutafuta usaidizi kutokana na aina ya mipayuko tunayoona ikielekezwa kwa vyombo vya habari. Hatutaruhusu watu kama Kuria kutumia utakatifu wa kumbi za Bunge kusafisha tabia zao mbaya," Sifuna alisema.

Kuria amekuwa akigonga vichwa vya habari tangu Jumatatu kufuatia maelezo yake ya dharau kwa kampuni ya Nation Media Group.

Mashambulizi hayo yalianza siku ya Jumapili wakati wa ibada ya kanisani, Waziri huyo alisema atamfuta kazi afisa yeyote wa serikali ambaye ataweka tangazo la biashara kwa idhaa zinazomilikiwa na kampuni ya Nation.

Alishutumu kampuni za vyombo vya habari kwa kueneza habari potovu kuhusu serikali.

Gadhabu za Kuria zilitokana na ufichuzi wa NTV, kudai kuwa baadhi ya mawaziri walihusika katika sakata ya kuagiza mafuta ya kupikia.

Hatua hiyo inadaiwa kumfanya mlipa ushuru kupoteza takriban Shilingi bilioni 5.6.

Akiongea baada ya kujibu maswali katika Seneti, Kuria alisisitiza kuwa hataomba msamaha wa kutoa matamshi yake dhidi ya vyombo vya habari.

Waziri huyo alisema amefanya kazi katika vyombo vya habari na amekuwa mmiliki wa vyombo vya habari hapo awali na anajua wakati chombo cha habari kinatumiwa.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved